Chelsea yampa Lionel Messi Sh1 bilioni kwa wiki

London, England. Chelsea imeripotiwa kwamba ishajiweka sawa na kukubali kumlipa supastaa Lionel Messi mshahara wa Pauni 1 milioni kwa wiki ili atue kwenye kikosi chao wakati ilipotenga ada ya Pauni 225 milioni kumsajili mwaka 2014.

Bilionea mmiliki wa klabu ya Chelsea, Roman Abramovich alikuwa tayari kuzama mfukoni na kutoa fedha nyingi ili kunasa huduma ya supastaa huyo wa Kiargentina baada ya kocha Jose Mourinho kumpigia simu staa huyo, kwa mujibu wa Gianluca di Marzio wa Sky Italy.

Bilionea huyo wa Russia pamoja na kocha Mourinho walikuwa tayari kutoa mkwanja wa kuvunja mkataba wa Messi na ilikuwa tayari kutoa mshahara wa Pauni 50 milioni kwa mwaka.

Ripoti zinadai kwamba Chelsea mara ya kwanza ilifanya mawasiliano na Messi Januari 2014 baada ya kesi yake ya mambo ya kodi.

Staa huyo alionyeshwa kuchoshwa na mamlaka za kodi za Hispania na jambo hilo liliwafanya The Blues kuamini kwamba wangeweza kutumia kama fursa ya kunasa saini yake.

Messi amuuliza rafiki wake wa zamani klabuni Barcelona, Deco kuhusu mtazamo wake wa kwenda kucheza Stamford Bridge, kabla ya kupigiwa simu kwa njia ya video na kocha Mourinho kupitia FaceTime.

Messi anaripotiwa alishawishiwa na Mourinho kwenye mazungumzo hayo na alikuwa tayari kwenda kucheza Chelsea na mambo yanadaiwa yalirahisishwa zaidi na Deco.