Lipumba akishinda kubadili mfumo stakabadhi ghalani

Muktasari:

Profesa Lipumba alisema hayo jana katika mkutano wake wa kampeni alioufanya viwanja vya kata ya Mangaka wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.

Nanyumbu. Mgombea urais wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema akichaguliwa kuwa Rais wa Tanzania, atabadilisha mfumo wa malipo ya stakabadhi kwa wakulima wa korosho.

Amesema mfumo uliopo unamuongezea umaskini mkulima, hivyo kutonufaika na kilimo.

Profesa Lipumba alisema hayo jana katika mkutano wake wa kampeni alioufanya viwanja vya kata ya Mangaka wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara.

“Wananchi wengi wa hapa Nanyumbu wanaolima korosho wamepewa umaskini wa makusudi, huu utaratibu wa stakabadhi umeongeza umaskini kwa wakulima. Nipeni kura zenu zote Oktoba 28 nikasimamie hili, nikawatetee wakulima wa korosho ili tukafanye mapinduzi ya kilimo,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema lengo la Serikali ya CUF ni kutaka kuona wafanyabiashara wakishindana kununua korosho kwa bei kubwa kutoka kwa mkulima.

Mgombea huyo alisema bidhaa hiyo inahitajika sana duniani, hivyo lazima mkulima awe na haki ya kuuza korosho zake kwa mtu atakayempa bei kubwa zaidi badala ya kusubiri kupangiwa.

“Nitahakikisha wakulima wa korosho wanakuwa na ushirika wao wenyewe wa kuuza korosho na sio wa kulazimishwa. Tunataka wapate bei nzuri ya mazao yao, tuzalishe korosho kwa wingi ziweze kutambulika nchini kote na nje ya nchi, ili mpate bei nzuri kwenye soko la dunia,” alisema.

Aliwaomba kura wananchi hao Oktoba 28, akisema ana lengo la kwenda kuwekeza kwenye kilimo hapo Nanyumbu na maeneo mengine nchini.

“Nitakomesha hii tabia ya wakulima wa korosho kuambiwa eti hawatalipwa fedha zao mpaka baadaye, hii kwangu haitawezekana.Nitahakikisha wanalipwa fedha zao kwa wakati, pia ipo michango ambayo wakulima wanaambiwa na wengine wanakatwa fedha zao bila kujua, hii kwangu haitatokea, nitahakikisha nawalinda wakulima wote nchini,” alisema Lipumba.

Naye mgombea ubunge wa jimbo hilo, Mussa Athman Mussa aliwaomba wananchi wamchague ili akamalize kero za wakulima wa korosho.

“Wakulima wa korosho hapa Nanyumbu hawathaminiwi maana na mimi nipo katika kundi la wakulima, hivyo naombeni ridhaa yenu ili nikawatetee wakulima wa korosho, nikapambane na kero ya stakabadhi ghalani kwa sababu imeletwa kwa ajili ya kuwadhulumu wananchi wa kati ambao hawajitambui

“Mkinichagua kuwa mbunge wenu nitahakikisha mkulima wa korosho anapeleka korosho yake kwenye ghala na kupata fedha zake hapo hapo,” alisema Mussa.

Alisema siku ya kupiga kura, wasifanye makosa, bali wamchague yeye akawatetee katika suala hilo na mengine na hatimaye wapate maendeleo katika jimbo hilo.

“Nichagueni kwa kura nyingi za Ndio ili nikawe mwakilishi wenu bungeni,” alisema.