Abdul Nondo azungumzia matatizo ya wanavyuo

Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo
Muktasari:
Aliyewahi kuwa mwenyekiti wa mtandao wa wanafunzi nchini, Abdul Nondo leo anatarajia kuzuru na kuzungumza na wananchi kwenye asasi ya Meza ya Duara mjini Kigoma ili kuwashukuru kwa kumuombea alipokuwa na kesi mahakamani.
Kigoma. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo amepanga kutembelea asasi ya kiraia ya Meza ya Duara mjini Kigoma kuwashukuru wananchi kwa kumuombea dua alipokuwa na kesi mahakamani.
Katibu wa Meza ya Duara, Juma Ramadhani amesema Nondo atafika ofisini hapo leo saa 10:30 jioni.
"Nondo alikuja hapa Meza ya Duara mwaka jana na kuomba tumuombee dua ili ashinde kesi yake, sasa leo anakuja kuwashukuru wananchi kwa kumuombea dua baada ya kupata ushindi mahakamani," amesema Ramadhani.
Amesema licha ya kutoa shukurani zake kwa wakazi wa Kigoma Ujiji, Nondo atazungumzia changamoto zinazowakabili wanafunzi wa vyuo vikuu nchini wanaojaribu kutetea na kupigania haki na demokrasia.
Ujio wa Nondo mjini Kigoma unaonekana kuvuta hisia za baadhi ya watu kwani wameahidi kufika kwa ajili ya kumsikiliza.
Mkazi wa Mwanga mjini Kigoma, Saimon Julius amesema Nondo amekuwa kivutio kwa jamii baada ya kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana na baadaye kukutwa akiwa mkoani Iringa akiwa hajitambui.
Mwisho.