Alichokisema Kikwete kuhusu CCM, Magufuli

Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Muktasari:

Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka wananchi kuchagua wagombea wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 kwa kuwa chama hicho tawala kina sera nzuri na kinazitekeleza.

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete amewataka wananchi kuchagua wagombea wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, 2020 kwa kuwa chama hicho tawala kina sera nzuri na kinazitekeleza.

Kikwete aliyekuwa rais mwaka 2005 hadi 2015 ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Oktoba 17, 2020 Mbagala jijini Dar es Salaam wakati akimuombea kura mgombea urais kupitia CCM, John Magufuli na kuwanadi wagombea ubunge wa chama hicho, Abdallah Chaurembo (Mbagala) na Doroth Kilave (Temeke).

Amesema sera nzuri za chama hicho zimeunganisha Taifa la Tanzania na kujenga umoja, undugu na upendo.

“Nchi yetu ina umoja amani na utulivu. Zipo nchi za wenzetu zinahangaika kuutafuta umoja utulivu na amani kwa sababu ukabila unawatafuna na udini wanawagawanya kutokana na maeneo wanayotoka,” amesema Kikwete.

Amesema yote yamewezekana tangu wakati wa Baba wa Taifa, Julius Nyerere na Abeid Aman Karume  na yanaendelea kutekelezwa hadi katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano.

Amesema CCM ina sifa ya kuchaguliwa kutokana na kuwa na ilani nzuri ya uchaguzi yenye changamoto zote zinazowakabili wananchi.

“Ukisoma ilani ya CCM kuna mapendekezo yanayoeleza namna ya kuzitatua na CCM imekuwa makini kuhakikisha ilani inatekelezeka,” amesema.

Amebainisha kuwa mwananchi anapokosea kuchagua kwa kipindi cha miaka mitano ni kama ameliwa kwa maelezo kuwa mwaka 2015 ajenda ilikuwa ni kupambana na rushwa na kukubaliana kutafuta mgombea asiyekuwa na makandokando.

“Chaguo letu la Magufuli hatukukosea hata kwenye ilani tuliandika ianzishwe mahakama maalum kwa ajili ya kupambana na rushwa na ndio maana kwenye uchaguzi huu sijamsikia mgombea yoyote akizungumzia masuala ya rushwa.”

 “Kazi kubwa imefanyika kwenye nyanja zote ninaposema hivyo sio kwamba mambo yameenda shwari kabisa lakini vituo vya afya viongezwe, hospitali ziongezwe na nyingine ziboreshwe kama ile ya moyo na figo pale Dodoma,” amesema Kikwete.

Kwa upande wa elimu Kikwete amesema licha ya idadi ya wanafunzi kuongezeka ubora wa elimu na ufaulu  umeongezeka katika shule za sekondari na vyuo vikuu.

Alibainisha kuwa endapo CCM itachaguliwa tena mambo mengine yatamaliziwa ikiwemo kuunganisha barabara kuu ambazo hazijamalizika kwa kuanzia pale zilipoishia.

Kikwete alieleza mkakati mwingine wa kupunguza msongamano baada ya kukamilisha barabara za juu ni kutengeneza miundombinu kwaajili ya usafiri.

“Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Wilaya ya Temeke ilinufaika na miradi mbalimbali chagueni tena wabunge wa CCM muendelee kunufaika msichanganye mbivu na mbichi.”

“Tumeelezwa zahanati zote za Wilaya zitakuwa vituo hayo ndio maelekezo ya chama, miaka mitano kazi kubwa ilifanyika tupeni tena miaka mitano ijayo tumalize na ahadi iliyopo ifikapo mwaka 2025 tatizo la maji liwe limeisha,” amesisitiza.