Basi lapata ajali Morogoro, 11 wajeruhiwa

Thursday January 9 2020

 

By Hamida Shariff, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Watu 11 wamejeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria la kampuni Kidinilo kuacha njia leo Alhamisi Januari 9, 2020 na kupinduka eneo la Mangae barabara ya Morogoro Iringa huku chanzo kikitajwa ni uzembe na mwendokasi.

Basi lililokuwa kilitokea Ifakara kwenda Dar es Salaam lilikuwa na abiria 68  kwamba majeruhi watatu hali zao sio nzuri kutokana na majeraha makubwa waliyoyapata na wamepelekwa katika hospitali ya rufaa mkoa wa Morogoro

Wakizungumza na Mwananchi, mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo ambaye pia ni mwenyekiti wa kijiji hicho, Alex Guge amesema ajali hiyo imetokea baada ya taili kupasuka huku dereva akiwa kwenye mwendo kasi kwenye eneo la kona.

Amesema baada ya kutokea kwa ajali hiyo yeye na wananchi wake walianza kuwatoa majeruhi walionasa pamoja na mizigo yao kisha kuimarisha ulinzi ili mizigo iwe kwenye usalama.

Naye mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo Charles Kidevu amesema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa dereva wa basi hilo na kwamba alikuwa akifukuzana na mabasi mengine kwa lengo la kuwahi kupakia abiria wa njiani.

Amesema dereva huyo alikuwa alianza kufukuzana na mabasi mengine baada ya kufika eneo la Mang'ula Kilombero.

Advertisement

Kwa upande wake, ofisa mfadhi wa Sumatra mkoa wa Morogoro, Andrew Mlacha amesema kabla ya kutokea kwa ajali hiyo alipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuwa dereva wa basi hilo alikuwa akiendesha kwa mwendokasi na kufukuzana na mabasi mengine kwa lengo la kuwahi abiria wa njiani.

Ofisa huyo amesema kabla ya kufanya mawasiliano na askari polisi kituo cha mabasi Ifakara alipokea taarifa ya ajali hiyo ambayo umesababisha basi hilo kuharibika vibaya.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro,  Wilbroad Mutafungwa  amemuagiza Kamanda wa kikosi Cha usalama barabarani mkoa wa Morogoro kumkamata dereva aliyesababisha ajali hiyo.

Amesema mazingira ya ajali hiyo yanaonyesha dereva wa ajali hiyo alivunja sheria kwa kuendesha mwendo wa kasi.

Advertisement