Bei mafuta ya kula kutoka nje juu

Muktasari:

Kwa mwezi mmoja uliopita, bei ya ndoo ya lita 20 ya mafuta ya kula imepanda kutoka Sh57,500 hadi Sh63,000 sawa na asilimia 9.5.

Dar es Salaam. Bei ya mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje imepanda hivyo huenda wananchi wakalazimika kuingia zaidi mifukoni.

Mabadiliko hayo ya bei yaliyotokea kwenye soko la dunia yanawalazimu waagizaji wa bidhaa hiyo nchini pia kupandisha ili kuepuka hasara.

Kwa mwezi mmoja uliopita, bei ya ndoo ya lita 20 ya mafuta ya kula imepanda kutoka Sh57,500 hadi Sh63,000 sawa na asilimia 9.5.

“Bei zimepanda kidogo tangu Septemba kutokana na mabadiliko katika soko la dunia,” alisema mkurugenzi wa kampuni ya East Coast Oil and Fats Limited, Gulam Dewji alipozungumza na The Citizen.

Kwa mwaka Tanzania inazalisha tani 200,000 za mafuta ya kula ingawa mahitaji yake ni tani 500,000 hivyo kuagiza tani 300,000 kutoka nje hasa mataifa Asia zaidi Malaysia na Indonesia.

Kukidhi mahitaji hayo, Serikali hutumia takriban dola 80 milioni kila mwaka kuagiza mafuta ya kula.

Ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya G&B Soap, Goodliving Makundi alisema bei imepanda kutokana na kutegemea zaidi mafuta kutoka nje ambako mabadiliko yakitokea lazima yaiguse Tanzania.

Vilevile, alisema ushuru wa forodha unaotozwa kwenye mafuta ghafi na yaliyochujwa nao unaongeza gharama kwa waagizaji hivyo kupandisha bei.

“Mafuta ghafi hutozwa asilimia 25 wakati yaliyochujwa ushuru wake wa forodha ni asilimia 35. Katika mazingira haya, bei lazima ipande ndio maana ndoo ya lita 10 iliyokuwa inauzwa Sh28,000 imepanda mpaka Sh34,000,” alisema.

Katika juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inahamasisha kilimo cha mazao ya mbegu kama chikichi na alizeti ili kuongeza uzalishaji wa mafuta ya ndani.

Mkurugenzi mtendaji wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Timothy Mmbaga alisema mabadiliko haya huenda yamechangiwa na mlipuko wa janga la corona.

“Hizi kampuni zinaajiri wataalamu hivyo kutokea kwa gonjwa hili kunaweza kusababisha kupanda kwa gharama za uendeshaji,” alisema Mmbaga.

Hata hivyo, akizungumzia mabadiliko hayo ya bei, naibu katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk Ludivick Nduhiye alisema wamelifuatilia na kujiridhisha kwamba hali si mbaya.

“Kuna kiasi kikubwa cha mzigo bandarini kinachosubiri kuingia na kusambazwa. Hakuna mabadiliko ya kodi kusema yameathiri uingizaji wa mafuta ya kula,” alisema.