Coco beach yafungwa, wauza mihogo waambiwa watafutwe kwingine

Muktasari:

Ufukwe wa Coco wafungwa ili kupisha uboreshaji wake, shughuli zilizokuwa zikifanyika ikiwemo uuzaji wa mihogo zasitishwa ili kupisha mchakato huo utakaodumu muda wa miezi sita.

Dar es Salaam. Kama wewe mlaji wa mihogo inayouzwa Coco Beach JIJINI Dar es Salaam nchini Tanzania sasa itakubidi utafute sehemu nyingine ya kupata huduma hiyo baada ya ufukwe huo kufungwa kwa miezi sita ili  kupisha uboreshaji.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Septemba 17, 2019 mkurugenzi wa halmashauri ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli amesema wametoa uamuzi huo baada ya mchakato wa manunuzi kwa mujibu wa sheria kukamilika.

Amesema mradi wa uboreshaji wa ufukwe huo utatekelezwa  kwa muda wa miezi sita na mkandarasi wa kampuni ya Tanzania Bulding Works aliyeshinda zabuni hiyo.

Kagurumjuli amesema baada ya kupatikana kwa mkandarasi huyo, ataanza kwa kuzungushia uzio wa mabati katika eneo na wale waliokuwa wakifanya shughuli zao katika eneo watalazimika kutafuta eneo jingine kwa kipindi hicho.

“Ndani ya miezi sita ufukwe huu utakuwa katika maboresho na utazungushiwa mabati, sasa tukiwaacha hivi ni nani atavuka mabati kwenda kununua mihogo?  Je usalama wao utakuaje wakati ujenzi ukiendelea,” amehoji.

“Wameshauriwa waende katika fukwe nyingine, maana bado tuna fukwe za Msasani, Ununio na  Dege Beach. Shughuli zote zilizokuwa zikifanyika eneo la Coco Beach zote zimesimama na wasubiri baada ya miezi sita, wakirudi eneo litakuwa bora zaidi,” amesema Kagurumjuli

Kwa mujibu wa Kagurumjuli mkandarasi huyo atajenga vitu mbalimbali ikiwemo viwanja vya michezo, mighahawa, kumbi za mikutano, nyumba za wageni, maeneo ya michezo ya ufukweni.

Meya wa Kinondoni, Benjamin Sitta amesma mradi huo ukikamilika wafanyabiashara hao watarudi katika eneo litakalokuwa limeboresha kwa mandhari nzuri ya kuvutia watu mbalimbali wakiwemo wateja wao.

“Tutachukua majina yao na watarudi na watafanya shughuli zao kwenye vibanda maalumu vilivyotengenezwa kisasa,” amesema Sitta.