DNA kutumika kutambua majeruhi ajali ya moto waliolazwa Muhimbili

Tuesday August 13 2019

 

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na mamlaka ya maabara ya mkemia mkuu wa Serikali ya Tanzania wameanza kufanya utambuzi wa vina saba (DNA) kuwatambua ndugu sahihi wa majeruhi waliopata  ajali ya moto iliyotokea Agosti 10, 2019 mkoani Morogoro.

Ajali hiyo ilitokea katika mtaa wa Itigi, Msamvu mkoani Morogoro baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.

Hospitali hiyo ilipokea majeruhi 46 kutoka hospitali ya Mkoa Morogoro kwa ajili ya matibabu zaidi hata hivyo hadi leo asubuhi wanane wamefariki dunia.

Lengo la kufanya hivyo ni kuondoa changamoto iliyojitokeza kwa baadhi ya ndugu kushindwa  kutoa maelezo sahihi hasa kwa majeruhi waliopo katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) ambao hawajaanza kujitambua.

Akizungumza na wanahabari leo Jumanne Agosti 13, 2019 mkuu wa kitengo cha mawasiliano ya umma MNH,  Aminiel Aligaesha amesema ili kutoa utata huo wameamua kupima sampuli kwa ajili ya utambuzi wa vinasaba (DNA).

 

Advertisement

“Tunashukuru ndugu wameanza kuja kuwaona ndugu zao waliopata ajali ya moto, lakini sasa imetokea changamoto katika utambuzi, kila mtu anaeleza la kwake huyu anasema amenyoa kiduku lakini ukiangalia wengi ni vijana wamenyoa hivyo tumeona ni bora tuwashirikishe wenzetu hawa ili kurahisisha utambuzi,” amesema.

Amesema mmoja wa majeruhi kati ya 39 waliokuwa wakipatiwa matibabu amefariki usiku wa kuamkia leo ambapo kwa sasa idadi ya majeruhi hospitalini hapo ni 38.

“Tulipokea wenzetu 46 lakini kwa bahati mbaya hadi sasa nane wameshapoteza maisha, kwa sasa wamebaki 38 ambapo kati yao 25 wanaendelea vizuri lakini 13 wapo ICU tuendeleeni kuwaombe ndugu zetu,” amesema.

Amesema miili saba kati ya nane imeshatambulika na imepelekwa Morogoro kwa ajili ya maziko huku mmoja ukihifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti MNH.

Naye maalamu kutoka ofisi ya mkemia mkuu wa Serikali,  Hadija Mwema amesema tayari sampuli zimeanza kuchukuliwa kwa wagonjwa walioko ICU kwa ajili ya kutambuliwa na ndugu zao.

Amesema sampuli ambazo zinaweza kutoa ulinganishi sahihi ni zile ambazo zimetoka kwa wazazi na watoto.

“Kitaalamu ni kwamba wazazi au watoto DNA zao zinarahisisha na zinauhalisia wa karibu zaidi kwa hiyo kama watakosekana hawa tutatumia ndugu wengine lakini ningependa watu wajue tu kuwa mama, baba na watoto wanatoa ulinganishi sahihi,” amesema Hadija

Advertisement