Dk Tenga, wenzake wamuandikia barua DPP kukiri makosa yao

Friday September 27 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Washtakiwa watano wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi akiwemo wakili, Dk Ringo Tenga wamemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini Tanzania (DPP) kuomba kukiri makosa yao.

Wakili wa washtakiwa hao, Byrson Shayo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Ijumaa Septemba 27, 2019 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.

Dk Ringo ambaye ni Mkurugenzi na mwanasheria wa kampuni ya Mawasiliano ya Six Telecoms Limited na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita, likiwemo la kutakatisha fedha na kuisababishia Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22.

Mbali na Dk Tenga, washtakiwa wengine ni Hafidhi Shamte au Rashidi Shamte ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Mfanyabiashara na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Peter Noni, Mkuu wa fedha wa kampuni hiyo Noel Chacha na Kampuni ya Six Telecoms.

Advertisement

Washtakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, Novemba 20, 2017 wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Mawakili wanaowatetea washtakiwa hao ni  Alex Mgongolwa, Semi Malima, Constancia Sospeter, Jeremiah Mtobesya na Bryson Shayo.

Katika kesi ya msingi, Dk Ringo na wenzake wanadaiwa kati ya Januari 1, 2014 na Januari 14, 2016 Dar es Salaam, walitoza malipo ya mawasiliano ya simu za kimataifa  chini ya kiwango cha Dola za Marekani  0.25 kwa  dakika kwa lengo la kujipatia faida.

Pia, katika kipindi hicho, wanadaiwa kuhujumu miundombinu ya TCRA kwa kutoza gharama chini ya kiwango na kushindwa kulipa kiasi cha Dola za Marekani 3,282,741.12 kwa TCRA, kama malipo ya mapato.

Washtakiwa hao wanadaiwa  katika kipindi hicho walishindwa kulipa ada za udhibiti za Dola za Marekani 466,010.07 kwa TCRA.

Katika shitaka la utakatishaji wa fedha, Hafidhi, Noni, Tenga na Chacha, wanadaiwa walitumia ama walisimamia Dola za Marekani 3,282,741.12 wakati wakijua fedha hizo ni zao la makosa ya udanganyifu linalotokana na mashtaka yaliyotangulia.

Vile vile ,washitakiwa hao wanadaiwa kuisababishia TCRA hasara ya Dola za Marekani 3,748,751.22.

Advertisement