Haya yalitikisa kwenye burudani

Muktasari:

Katika kipindi kisichopungua miezi sita ambacho tovuti ya Mwananchi ilipokuwa ikitumikia adhabu iliyopewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) yaliibuka matukio mbalimbali ya kuvutia katika tasnia ya burudani.

Katika kipindi kisichopungua miezi sita ambacho tovuti ya Mwananchi ilipokuwa ikitumikia adhabu iliyopewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) yaliibuka matukio mbalimbali ya kuvutia katika tasnia ya burudani.

 Alikiba arejea nyumbani

Julai 30 Alikiba alirudi nyumbani kwao Kigoma kwa staili ya aina yake. Alipiga Bonge la Shoo katika Uwanja wa Lake Tanganyika, shoo iliyobatizwa jina la ‘Home Coming concert’.

Mbali na shoo pia Alikiba alitoa msaada kwenye kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, msaada ambao alikusanya kutoka kwa wadau na mashabiki wake.

Jambo la CCM Uhuru

Chama cha Mapinduzi kilikuja na kitu cha tofauti upande wa burudani kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaama kwa kuandaa shoo ambayo ilipandisha zaidi ya wasanii 200 jukwaani.

Shoo ilifanyika Uwanja wa Uhuru Agosti 15 na kuhudhuriwa takribani wakazi 30,000 wa Dar es Salaam ambao kiu yao ya burudani ilikatwa na list ndefu ya wasanii; kuanzia Rayvann, Zuchu, Marioo mpaka kwa waigizaji kama Wema Sepetu na wachekeashaji kama Ringo.

Simba Day

Katika kusherehekea Simba day alialikwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Diamond Platnumz. Jamaa kama kawaida yake hakuingia kinyonge hapo Uwanja wa Mkapa, alitua na chopa kisha akapiga bonge moja la shoo na kupelekea akawa BIG STORY mjini wiki nzima.

Unaambiwa Mondi alipiga shoo iliyompandisha mzuka muwekezaji wa timu, Mohamed Dewji ‘Mo’ kiasi kwamba alishuka alipokuwa amekaa akaja kujiunga na Diamond jukwaani na kuanza kucheza mpaka akavua shati — ilikuwa noma unaambiwa.

Mbali na Diamond pia wasanii wengine kama vile Meja Kunta, bendi ya Twanga pepeta na Marioo walinogesha tukio hilo lililofanyika Agosti 22.

Shoo ya Wanawake pekee

Basi bwana, tulivyokuwa offline, staa wa muziki wa malavidadi, Juma Jux naye akaandika historia kwa kupiga shoo maalum kwa ajili ya watoto wa kike tu.

 

Yaani katika shoo hiyo iliyofanyika Agosti 28 katika ukumbi wa Hyatt Regency Dar es Salaam, walikuwa wanaruhusiwa kuingia mademu tu huku pia kila kitu humo ndani kikifanywa na wanawake, kaunzia wahudumu, walinzi na zaidi. Mwanaume pekee aliyekuwepo humo ndani alikuwa ni Jux na baadhi ya wasanii aliowaalika kama vile Joh Makini.

 

Siku ya Mwananchi

Yaani Simba wafanye tukio kubwa, Yanga watulie tu, haiwezekani. Basi baada ya Simba kufanya kufuru siku ya Simba Day kwa kumualika Diamond Platnumz ambae alitua na helkopta, Yanga nao wakafanya bonge la sapraizi kwa kumualika Konde Boy Harmonize na akaingia kijeda akining’inia kwenye kamba.

Konde Boy alikuwa na jukumu zito la kuingia uwanja wa Mkapa kwa staili ambayo pengine inaweza kumfunika ya Diamond Platnumz aliyeingia na helkopta bila kutarajiwa. Kwa sababu hiyo, Konde Boy aliingia akining’inia juu ya kamba kama mwananjeshi — na tukio hilo lilibamba mitandaoni huku pia gumzo ikiwa ni mabishano ya pande mbili kwamba Harmonize alianguka wakati anashuka kwenye ile kamba.

Mbali na Harmonize, pia wasanii kama Shilole, Baba Levo, G Nako, Bilnas, Sholo Mwamba na wengine walitumbuiza katika siku hiyo Agosti 30.

Miaka 20 ya Jaydee

Kabla hatujafungiwa, Lady Jaydee alikuwa na plan kwamba atafanya shoo za kuadhimisha miaka 20 kwenye gemu, na shoo hizo atazifanya Tanzania nzima kwa kuzunguka kwenye mikoa mingi. Hata hivyo wakati anaanza tu, mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19 ukatokea, akashindwa kuendelea.

Hata hivyo hali ilipotulia akendelea tena, na shoo kubwa zaidi alifanya Dar es Salaam katika ukumbi wa Mlimani City, shoo ambayo alisindikizwa na wasanii wengine kama vile Zuchu, Maunda Zoro, Mwasiti, T.I.D na Domokaya.