VIDEO: Ilivyokuwa safari ya mwisho ya Mkapa

Muktasari:

Moja ya tukio kubwa lililotokea kipindi ambacho Tovuti ya Mwananchi pamoja na mitandao ya kijamii kufungiwa kwa miezi sita ni kifo cha Rais wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Dar es Salaam. Moja ya tukio kubwa lililotokea kipindi ambacho Tovuti ya Mwananchi pamoja na mitandao ya kijamii kufungiwa kwa miezi sita ni kifo cha Rais wa awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Mkapa alizaliwa kijiji cha Lupaso mkoani Mtwara Novemba 12, 1938 kisha kupitia hatua mbalimbali za kimaisha hadi kuwa Rais wa Tanzania. alifariki dunia Julai 24, 2020 na kuzikwa kijijini Lupaso Julai 27,  2020 mazishi yaliyoshuhudiwa na viongozi wa ndani na nje ya nchi ya Tanzania walioongozwa na Rais John Magufuli.

Safari ya maisha yake ya miaka 81 duniani imejumuisha utumishi uliotukuka kwa umma hata kumfanya ashike wadhifa wa urais kwa miaka 10 kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005.

Alifariki kutokana na tatizo la moyo kusimama kufanya kazi. Alikutwa na kifo akiwa amelazwa hospitalini jijini Dar es Salaam alikokuwa anatibiwa ugonjwa wa malaria.

Mwili wa Mkapa ulifikishwa Lupaso, kijiji kilichopo wilayani Masasi kwa kutumia helkopta ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) baada ya kuagwa jijini Dar es Salaam.

Ibada ya mazishi ilianza saa 1.30 asubuhi ikiongozwa na rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), Gervas Nyaisonga ambaye alitoa salamu za kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis.

Akitoa mahubiri katika ibada hiyo, Askofu wa Jimbo Kuu la Songea, Damian Dallu alisema Mkapa amemaliza mwendo wake kwa kuonyesha moyo wa toba alipotoa kitabu chake cha `My life, My Purpose’ (Maisha yangu, kusudi langu).

Mbali na viongozi wa dini, walikuwepo marais wastaafu, ambapo wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alieleza jinsi alivyomfahamu Mkapa tangu alipokuwa mbunge wa Nanyumbu baadaye akamrithi katika nafasi ya urais.

Kwa upande wake, Rais Ali hassan Mwinyi aliyeiongoza Tanzania katika awamu ya pili aliwataka waombolezaji kumwombea hayati Mkapa msamaha kipindi hiki anapomaliza safari yake.

“Mwanadamu kwa maumbile yake ni mkosaji na ndugu yetu ni mwanadamu kama walivyo wanadamu wengine.

“Huenda, katika umri wake amewahi kuteleza, akafanya kosa asilotaka, asilolipenda. Katika hali kama hii mwenzenu akiondoka ulimwenguni, jambo la kwanza ni kumwombea msamaha kwa Mwenyezi Mungu, endapo alikosea,” alisema Mwinyi, ambaye wakati wa utawala wake, alimteua Mkapa kuwa waziri katika wizara tatu tofauti ikiwamo ya Mambo ya Nje, Habari na Utangazaji na Elimu ya Juu, Sayansi na Tekinolojia.

Awali wananchi kijijini walipewa fursa ya kuuaga mwili wa Mkapa  tangu saa 3:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana Rais Magufuli alipoingia uwanjani hapo.

Mkapa aliusia azikwe Lupaso

Akizungumza kuhusu mazishi hayo, Rais Magufuli alisema Mkapa ndiye aliyechagua kuzikwa kijijini hapo.

“Kuna wakati Serikali ilipanga mahali pa maziko kwa viongozi na tulipangiwa kuwa tunazikwa Dodoma kwa sababu ndiyo makao makuu. Miaka miwili mitatu, Mzee Mkapa akaniuliza, mlipanga maziko yawe Dodoma? Mimi msinizike Dodoma. Nikamuuliza wewe wapi? Mimi Lupaso.

“Nikamuuliza Mzee Kikwete, akasema mimi Msoga. Nikaogopa kumuuliza mzee Mwinyi kwa sababu alikuwa na miaka 90 na kitu, nikaona nikimuuliza halafu likatokea la kutokea nitaonekana nimeleta uchuro. Lakini mimi kwa dhamira yangu, nikasema nitazikwa Chato,” alisema Rais Magufuli.

Alisema eneo hilo lililotengwa kwa mazishi ya viongozi atapewa Waziri Mkuu mstaafu, John Malecela kwa sababu anaishi Dodoma na linalobaki watapewa wananchi.

“Aliyeanzisha huo utaratibu ni Mzee Mkapa, kwa hiyo Mkapa alipenda kwao. Kwenye hili tujifunze. Mzee Mkapa angeweza kuzikwa Dar es Salaam, ana eneo kubwa tu na shamba kubwa pia.

“Angeweza kuzikwa Lushoto au eneo jingine lolote, lakini ndani ya dhamira yake alitaka azike kijijini kwake. Tujifunze kwa upendo mkubwa aliouonyesha kwa wananchi wake,” alisema Rais.