Jeshi la Magereza Tanzania kuanza kujitegemea

Wednesday February 19 2020

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini Tanzania, Kamishna Jenerali Suleiman Mzee amesema kuanzia Machi Mosi, 2020 Magereza zote nchini zitaanza kujitegemea kwa asilimia mia moja kwa chakula cha wafungwa na huduma nyinginezo.

Amesema uamuzi huo ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Tanzania, John Magufuli ambaye mara kadhaa amekuwa akiagiza Magereza nchini kujitegemea kwa kuwatumia wafungwa kufanya shughuli mbalimbali za kilimo.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Februari 19, 2020 mjini Dodoma katika kikao kazi cha maofisa waandamizi wa jeshi hilo kutoka mikoa yote Tanzania Bara kwa ajili ya kupeana mikakati ya namna ya kufanikisha mpango wa kujitegemea.

“Magereza kujitegemea inawezekana kwani tunazo rasilimali nyingi ikiwemo mashamba ya kilimo, mifugo, wataalam wa kutosha na nguvu kazi ya wafungwa. Tukisimamia vizuri na kuachana na ubinafsi tutaliwezesha jeshi letu kujitegemea,” amesema  Kamishna Jenerali Mzee.

Amewataka  wakuu wote wa Magereza kuhakikisha  wanaanza kujitegemea, “kuanzia Machi Mosi kila mkuu wa magereza ahakikishe  anajitegemea katika mkoa wake na lazima mkubali kufanya mabadiliko haya bila visingizio. Atakayeshindwa kujitegemea nitamwajibisha mara moja.”

Amebainisha kuwa tayari ameanza maandalizi ya ujenzi wa ofisi za makao makuu ya jeshi hilo pamoja na nyumba za watumishi jijini Dodoma kwa kutumia rasilimali mbalimbali.

Advertisement

Kikao kazi cha maofisa waandamizi wa Magereza ndio kikao cha juu cha uongozi  kinachowakutanisha maofisa waandamizi kutoka makao makuu, wakuu wa magereza wa mikoa, wakuu wa vyuo, mkuu wa kikosi maalum na mkuu wa Sekondari Bwawani.

Advertisement