Kauli ya waziri, CCM yatofautiana uchaguzi serikali za mitaa

Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo

Muktasari:

Wapinzani wanalalamikia kanuni za uchaguzi huo kuchelewa, wakati kiongozi mmoja wa CCM alisema walishapata kanuni hizo na wanajua umepangwa kufanyika Novemba 24.


Dar es Salaam. Kwa kawaida uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa hufanyika takriban mwaka mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu, lakini kutotangazwa kwa kanuni hadi sasa kumefanya kila chama cha siasa kusema lake.

Wapinzani wanalalamikia kanuni za uchaguzi huo kuchelewa, wakati kiongozi mmoja wa CCM alisema walishapata kanuni hizo na wanajua umepangwa kufanyika Novemba 24.

Juzi, Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo alijitenga na kauli hiyo ya chama chake akisema hakuna anayejua tarehe wala kanuni za uchaguzi huo muhimu wa ngazi ya mwanzo unaoigusa jamii moja kwa moja.

Alikua akipingana na kauli iliyotolewa Agosti 7 na katibu wa oganaizesheni ya sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM, Pereira Silima.

Siku hiyo, Silima aliliambia Mwananchi kuwa tayari wameshapatiwa kanuni pamoja na ratiba inayoonyesha kuwa uchaguzi huo utafanyika Novemba 24.