Kiba: Siwezi kuhudhuria tamasha la Diamond natafuta mafanikio yangu

Friday November 8 2019

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ali Kiba amesema hana ugomvi na Diamond Platnumz ila hawezi kushiriki kwenye tamasha lake kwa sababu na yeye anatafuta mafanikio.

Kiba amelazimika kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo mara ya pili, wiki iliyopita Diamond alisema uongozi wa lebo ya WCB unafanya mazungumzo na Kiba ili akatumbuize kwenye tamasha la Wasafi linalofanyika kesho kwenye viwanja vya Posta Kijitonyama Jijini Dar es Salaam, Tanzania.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kiba ameandika akimtaka Diamond kutomfuatilia akitumia neno “unikome.”

Akizungumza na waandishi wa habari leo jioni Novemba 8, 2019, Kiba amesema, “Ninamuheshimu kwa namna anavyoutangaza muziki, lakini siwezi kutumbuiza kwenye tamasha lake kwa sababu na mimi natafuta mafanikio yangu, ”amesema Kiba.

Amesema atafanya  ziara aliyoiita ‘Unforgatable’ nchini nzima akiweka kambi za kupima afya kila mkoa kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

“Pia tutatoa elimu juu ya ugonjwa wa Ebola,” amesema Kiba.

Advertisement

 

Advertisement