Breaking News

Lissu: Kapigeni kura tubadilishe mfumo utawala wa nchi ya Tanzania

Saturday October 17 2020

By Peter Elias, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mgombea urais wa Tanzania kupitia  Chadema, Tundu Lissu amewataka wananchi kwenda kupiga kura Oktoba 28 ili kuuondoa madarakani utawala wa CCM uliodumu tangu Tanzania ipate uhuru.

Lissu ameyasema hayo leo, Oktoba 17 zikiwa zimebaki siku 10 tu kabla ya siku ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 28. Ameyasema hayo kwenye mkutano wake wa kampeni uliofanyika wilayani Manyoni akielekea Kongwa halafu Dodoma mjini.

Mgombea huyo amesema uchaguzi wa mwaka huu ni muhimu kuliko wakati wowote kwa sababu utaundaSerikali itakayolinda uhuru, haki na maendeleo ya watu.

"Katika hizi siku 10 zilizobaki, hakikisheni mnahamasishana kwenda kupiga kura ili mfanye mabadiliko ya utawala wa nchi yenu," amesema mgombea huyo.

Lissu amewataka wananchi wakapige kura kuchagua uhuru wa kuwasema viongozi waliowachagua na kuwakosoa pale wanapokosea.

"Mkachague chama kitakacholinda uhuru wenu, lazima muwakosoe viongozi mliowachagua," amesema Lissu na kushangiliwa.

Advertisement

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Manyoni kupitia Chadema, Aisha Luja ameahidi kutatua kero ya maji inayowakabili wananchi kwa muda mrefu.

"Ndugu zangu mkituchagua tutahakikisha mnapata maji safi na salama. Serikali ya Chadema itasimama nasi katika changamoto tulizonazo," amesema Luja.

Advertisement