Madereva watoa siku saba kwa wamiliki wa Uber, Taxify

Thursday December 19 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Chama cha madereva wa usafirishaji kwa njia ya mtandao (Toda) kimetoa siku saba kukutana na wamiliki wa kampuni za huduma ya usafiri kwa njia ya mtandao za  Uber na Taxify ili kujadiliana kuhusu changamoto zinazowakabili madereva.

Kimesema kama itashindikana kukutana na wamiliki hao watawafungulia kesi mahakamani.

Toda imetoa kauli hiyo baada ya kuibuka kwa madai kuwa wamiliki hao wanachukua asilimia kubwa katika kila safari anayofanya dereva, kushusha bei za safari kila siku bila kuzingatia gharama za usafirishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 19, 2019 mwenyekiti wa Toda, Linus Chuwa amesema awali biashara hiyo ilikuwa ikivutia kampuni nyingi na kipato kilikuwa kizuri lakini kwa sasa hali ni  tofauti.

“Wakati kampuni hizi zinaanza biashara nchini benki nyingi ikiwemo CRDB zilivutiwa kutoa mikopo ya magari kwa madereva ambayo walikuwa wakiilipa kwa miaka miwili lakini sasa suala hilo limekuwa gumu kutokana na bei za usafirishaji kuwa ndogo,” amesema Chuwa

Amesema wakati mwingine ni ngumu kujua dereva anavyoumia kwa kuwa kampuni hizo hazimiliki magari na baadhi ya madereva waliokopa wakishindwa kulipa madeni na magari yao kupigwa mnada.

Advertisement

“Tumekuwa kimya kwa muda mrefu, tumelia tumeumizwa lakini hivi sasa tuseme basi kwa sababu hata kile kidogo tulichokuwa tunatarajia kukipata hakipo,” amesema Chuwa.

Mwenyekiti wa kamati ya usuluhishi wa Toda, Ebony Ford amesema kampuni hizo zinachukua asilimia 25 kwa Uber na asilimia 20 kwa Taxify katika kila safari na kwamba madereva wana mahitaji mengi ya msingi ili kuendesha vyombo hivyo.

“Wao ndio wapangaji wa bei zote ambazo dereva anafanya na abiria wake, wamekuwa wakishusha mara kwa mara bila kuzingatia gharama ambazo dereva anatumia. Wakati kampuni hizi zinaingia nchini bei kwa kilomita moja Sh950 na abiria alilipa Sh150 kwa kila dakika ya safari lakini sasa kilomita moja ni  Sh450 na mteja analipa Sh80 kwa kila dakika ya safari.”

“Hili ni punguzo la zaidi ya asilimia 50 kwa bei katika kila kilomita na zaidi ya asilimia 40 ya bei katika kila dakika kweli madereva watawezaje kumudu gharama za kulipa madeni na kuendesha maisha,” amesema Ford

Mmoja wa madereva, Abdallah Suleiman ameiomba Serikali kuingilia kati ili waweze kupewa mikataba inayowanufaisha wote.

Advertisement