Magufuli kuwashukia viongozi watakaoshindwa kuhamasisha uandikishaji Serikali za mitaa

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka viongozi wa mikoa kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewataka viongozi wa mikoa kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Amesema wanapaswa kuchangamka kwa kuwa mwisho wa uandikishaji ni Oktoba 14, 2019, kwamba ambao mikoa yao itaandikisha watu wachache, hatua atakazochukua hadhani kama atalaumiwa na Watanzania.

Ametoa kauli hiyo siku moja baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo kuahidi kupeleka pendekezo maalum kwa mikoa itakayofanya vibaya katika uandikishaji wakati akitoa taarifa za zoezi hilo jana mkoani Katavi mbele ya kiongozi mkuu huyo wa nchi.

Leo Magufuli wakati akizungumza katika uzinduzi wa safari za ndege za Shirika la Ndege Tanznaia (ATCL) mkoani Katavi, Rais Magufuli amesema atawashangaa viongozi wa mikoa itakayofanya vibaya.

 “Jana Waziri alitoa takwimu za baadhi ya mikoa iliyofanya vizuri. Ninafuatilia lakini alitoa baadhi ya mikoa inayoendelea kufanya vibaya. Zoezi likikamilika nitataka Waziri anipe taarifa za mikoa iliyofanya vizuri na iliyofanya vibaya.”

“Nataka niseme hapa hadharani, ile mikoa ambayo watu wao watashindwa kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kupiga kura nitawashangaa. Ninajua Watanzania hawatanilaumu kwa hatua zitakazochukua,” amesema Magufuli.