Mahakama kutoa hukumu kesi ya DC Chemba anayetaka kutaliki

Friday August 23 2019

 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga, Dar es Salaam nchini Tanzania leo Ijumaa Agosti 23,2019 itatoa hukumu katika kesi ya madai ya talaka iliyofunguliwa na Mkuu wa Wilaya ya Chemba (DC), Simon Odunga dhidi ya ndoa ya serikali aliyoifunga na Ruth Osoro.

Hukumu hiyo itatolewa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Elia Mrema mara baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili na kufunga ushahidi wao.

Kwa mujibu wa kesi hiyo, Odunga ambaye ni mdai alitoa ushahidi mwenyewe hakuwa na mashahidi.

Ruth ambaye ni mdaiwa yeye alitoa ushahidi wake na akawa na mashahidi wawili akiwepo dada yake na Medilina Mbuwuli ambaye ni mke mwenza wa ndoa ya Kikristu wa Odunga.

Ndoa ya Odunga na Ruth inadaiwa kufungwa Februari 21, 2010 na kupata cheti cha ndoa B no 0979341.

Katika kesi hiyo Odunga analalamikiwa na mkewe Ruth kwa kutokutoa mafunzo ya mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka minne kwa kipindi cha miaka mitatu.

Advertisement

Licha ya malalamiko hayo ikiwamo kutelekezwa, kunyanyaswa na kupewa vitisho Ruth anaomba Mahakama isivunje ndoa yake kwa kuwa bado anampenda mume wake huyo.

Kwa upande wa Odunga yeye anaomba mahakamani  ivunje ndoa hiyo na iamuru   apewe ridhaa ya kumlea mtoto wao  wa kiume mwenye umri wa miaka minne bila bugudha yoyote.

Katika kesi hiyo, Odunga anaomba kutoa talaka kwa mkewe huyo kwa sababu amechoshwa na magomvi na kudhalilishwa sehemu zake za Kazi.

Baada ya kesi hiyo kusikilizwa  kwa ushahidi wa pande zote na kufunga ushahidi wao, Hakimu Mrema aliwapa nafasi ya kutoa mapendekezo endapo mtoto huyo atatakiwa kuishi na mama yake.

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga alipendekeza kutoa kiasi cha  Sh50,000 kwa mwezi kama fedha ya chakula kwa mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 4 aliyezaa na Ruth Osoro.

Hata hivyo,  Odunga alidai kuhusu matibabu ya mtoto ana bima ya afya na kwamba kuhusu elimu anaomba mahakama impatie mtoto huyo atamsomesha kwa kadiri anavyoona inafaa na kwa uwezo wake. Na kwamba atahusika kwa asilimia 100.

Hata hivyo, Ruth alipinga kiwango hicho kuwa ni kidogo na kwamba hakiwezi kukidhi chochote.

Hivyo aliiomba mahakama iamuru apeleke risiti ya mshahara wake ili iweze kuangalia ni kiwango gani kitakidhi kumtunza mtoto.

Hata hivyo, hakimu Mrema alimtaka apendekeze kiwango Ruth alidai kuwa kiwango cha Sh50,000 kwa hadhi yake maana hata msukuma mkokoteni anakimudu na kupendekeza kiwango cha Sh1 milioni.

Kwa upande wake, Odunga alipinga kiwango cha Sh1 milioni na kueleza Ruth hajui kipato chake hicho kiwango alichokipendekeza ni kikubwa kulingana na kipato chake hawezi.

Hata hivyo, Odunga alidai anapendekeza kiwango hicho kwa sababu ana watoto wengine watatu wanahitaji awahudumie hivyo  aliiomba atoe Sh50,000 kwa mwezi.

Odunga aliomba apewe mtoto amlee na iwapo itashindikana basi awe huru kumtembelea bila kikwazo chochote.

Soma zaidi

Advertisement