Mahakama yakataa ushahidi wa bosi PPRA

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu imekataa kupokea vielelezo vya nyaraka za ripoti ya ukaguzi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) vitumike katika ushahidi kwa kuwa hazina mihuri ya moto.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu imekataa kupokea vielelezo vya nyaraka za ripoti ya ukaguzi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) vitumike katika ushahidi kwa kuwa hazina mihuri ya moto.

Hayo yametokea leo Jumatano Machi 25, 2020 baada ya wakili wa utetezi, Peter Kibatala  kuiomba mahakama kutopokea vielelezo hivyo vilivyotolewa na shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka kwa kuwa nyaraka hizo zilikuwa na upungufu ikiwemo  kutoonyesha mihuri ya moto katika kurasa zilizowasilishwa.

Shahidi huyo  ambaye ni ofisa mtendaji mkuu wa PPRA, Dk Laurent Shirima katika kesi ya kuisababishia Serikali hasara ya Dola 527, 540 za Marekani inayowakabili vigogo wawili wa Kampuni Hodhi ya Mali za Reli (Rahco) alitoa ushahidi wake  na kuiomba mahakama hiyo ipokee vielelezo hivyo vitumike katika ushahidi wake.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema nyaraka  zilizowasilishwa zilikuwa hazionyeshi mihuri ya moto.

"Moja ya masharti inatakiwa kila ukurasa ionyeshe mihuri ya moto lakini katika kurasa zote mihuri iliyopo haionyeshi hivyo nyaraka hizi zina upungufu hazitapokelewa katika mahakama hii," amesema Simba.

Simba aliahirisha shauri hilo hadi Aprili Mosi, 2020 litakapokuja kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Rahco,  Benhardard Tito; Mwanasheria wa zamani wa Kampuni hiyo, Emanuel Massawe na mwakilishi wa Kampuni ya Rothschild South Afrika proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma.