Mahakama yatoa neno kesi ya Ndama Mtoto wa Ng’ombe

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi ya kughushi kibali cha madini ya Dola 8 milioni za Marekani inayomkabili mfanyabiashara, Ndama  Hussein ‘Pedeshee Ndama Mtoto ya Ng’ombe’ kukamilisha upelelezi

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeutaka upande wa mashtaka katika kesi ya kughushi kibali cha madini ya Dola 8 milioni za Marekani inayomkabili mfanyabiashara, Ndama  Hussein ‘Pedeshee Ndama Mtoto ya Ng’ombe’ kukamilisha upelelezi.

Upande wa mashtaka umetakiwa kukamilisha upelelezi kwa kuwa shauri hilo lipo kwa zaidi ya miaka mitatu.

Hatua hiyo imekuja baada ya wakili wa Serikali, Jenipher Masue kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Maira Kasonde  kuwa shauri hilo limekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado haujakamilika.

Baada ya maelezo hayo yaliyotolewa leo Ijumaa Julai 12, 2019 wakili wa utetezi, Nashwar Nkungu amedai shauri hilo lipo tangu mwaka 2016 na upande wa mashtaka waliieleza faili lipo kwa mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kuomba mahakama itoe tamko la mwisho.

Hakimu Kasonde amekubaliana na  upande wa utetezi na kushauri upande wa mashtaka kutumia busara au kukamilisha upelelezi.

"Upande wa mashtaka tunawapa nafasi tena shauri linapofika mahakamani ndani ya siku 60 upelelezi unatakiwa kukamilika lakini hili shauri lipo zaidi ya miaka mitatu hakikisheni siku shauri hili linapokuja mahakamani mje na majibu," amesema  Kasonde.

Ndama anakabiliwa na mashtaka matano ya  kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Miongoni mwa mashtaka yanayoendelea kumkabili, Ndama anadaiwa Februari 20, 2014 Dar es Salaam, alighushi nyaraka ya kibali cha kusafirisha madini na sampuli za madini kwa kusudi la kuonesha kuwa kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited iliruhusiwa kusafirisha maboksi manne ya dhahabu yenye kilogramu 207 yenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000.00 kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited wakati akijua si kweli.

Pia anadaiwa Machi 6, 2014, Dar es Salaam, alighushi kwa kutengeneza hati ya kibali ya Umoja wa Mataifa ofisi ya Dar es Salaam akijaribu kuonyesha kilogramu 207 za dhahabu kutoka nchini Congo zinatarajiwa kusafirishwa na kampuni ya Muru Platnum Tanzania Investment Company Limited kwenda Australia kwa kampuni ya Trade TJL DTYL Limited, zimesafirishwa bila jinai yoyote wakati akijua si kweli.

Pia anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi fomu ya forodha yenye namba za usajili R.28092 akionyesha kampuni ya Muru imeilipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) dola za Marekani 331,200 kama kodi ya uingizaji wa bidhaa ambazo zina uzito wa kilogramu 207 za dhahabu zenye thamani ya Dola za Marekani 8,280,000 kutoka Congo.

Shtaka lingine anadaiwa Februari 20, 2014, alighushi nyaraka ya bima kutoka Phoenix of Tanzania Assurance Company Ltd akionyesha kampuni ya Muru imeyawekea bima maboksi manne yaliyokuwa na dhahabu hizo.

Anadaiwa kati ya Februari 26 na Machi 3, 2014, Dar es Salaam kwa njia ya udanganyifu alijipatia kutoka kwa kampuni ya nchini Australia ya Trade TJL DTYL Limited Dola za Marekani 540,000 baada ya kudanganya atawapa na kusafirisha dhahabu hizo.