Majaliwa aanza na bei ya saruji

Monday November 16 2020
majaliwa pic

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema baada ya kuapishwa kwake, ataanza kushughulikia bei ya saruji ambayo inaonekana kupanda katika maeneo mengi nchini.

Amewataka wakuu wa mikoa hadi Novemba 20, 2020 wawe wamekwenda kwenye viwanda vya kuzalisha saruji na mawakala kuangaalia sababu ya kupanda kwa bidhaa hiyo.

Majaliwa amesema katika jitihada zilizofanywa na Serikali katika eneo la uboreshaji wa miundombinu, bei  ya saruji haikutakiwa kupanda.

“Inawezekana walijisahau wakidhani Serikali ipo katika uchaguzi haiwezi kufanya jambo lolote.  Nakuhakikishia Rais kuwa nataka kuanza na hilo,”

 “Kitu kizuri ni kuwa wakuu wa mikoa wako hapa, niwaagize na wao hadi Novemba 20, 2020 saa 4 asubuhi kila mmoja aende katika kiwanda cha saruji, mawakala waangalie kwa nini bei imepanda kutoka bei ya kawaida hadi ongezeko la Sh3,000, Sh4,000 bila sababu yoyote,”amesema na kuongeza:

“Wakati Serikali haijaongeza hata kodi, miundombinu ipo, waliotaka gesi tumewapelekea, waliotaka makaa ya mawe wamepatiwa sasa bei kwa nini imepanda kwa kiasi hicho, tunahitaji maelezo hayo,” amesema Majaliwa

Advertisement

 

 

Advertisement