Majaliwa ajiandikisha kupiga kura, awaonya wapotoshaji

Muktasari:

Shughuli ya uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Tanzania utakaofanyika Novemba 24, 2019 ulioanza Oktoba 8 utamalizika Oktoba 14, 2019.

Ruangwa. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amejiandikisha katika daftari la wapiga kura wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019.

Majaliwa na Mkewe, Mary Majaliwa wamejiandikisha leo Jumamosi Oktoba 12,2019 katika kituo cha shule ya msingi Nandagala, wilayani Ruangwa mkoani Lindi.

Waziri Mkuu ametumia nafasi hiyo kuhamasisha kujitokeza kwa wingi na kupuuza upotoshaji wa kadi za uchaguzi mkuu kwamba zitatumia uchaguzi wa serikali za mitaa.

Miongoni mwa sifa za mtu anayetakiwa kujiandikisha kwa ajili ya kuchagua kiongozi ngazi ya Kijiji, Kitongoji au mtaa kupitia uchaguzi huo ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania, mwenye umri miaka 18 au zaidi, awe na akili timamu.

Pamoja na sifa hizo, mgombea atalazimika kuwa na umri unaoanzia miaka 21 au zaidi na awe raia mwenye shughuli ya kujipatia kipato.

Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, Waziri Mkuu amesema shughuli ya kujiandikisha ni ya kitaifa inayowezesha kuchagua kiongozi umtakaye au kugombea katika uchaguzi huo.

"Kila mmoja anapaswa kuja kujiandikisha. Zoezi hili ni tofauti na lile la uchaguzi mkuu. Kuna watu wanafanya upotoshaji wa makusudi, wanawadanganya wenzetu kwamba kama una kadi ya uchaguzi huna haja ya kujiandikisha. Hii siyo kweli, hiyo kadi ni ya uchaguzi wa mwakani," amesema.

"Tunatakiwa tuchague viongozi watakaosimamia maendeleo, wanaohamasisha maendeleo. Tunatakiwa tuchague viongozi ambao ni waadilifu, waaminifu, wachapakazi, wasikivu, wapenda watu na wanaoweza kusimamia fedha zinazoletwa hapa. Ninyi mnawafahamu kwa sababu mnaishi nao.”

Amesema Serikali imetoa fedha za kununua taa za barabarani, zitakazofungwa ili kufanyika biashara kwa wakati wote hadi usiku.

"Tunaboresha vijiji vyetu kuanzia Nanganga, Nangumbu, Michenga (Misri), Michenga (Jerusalem), Chimbila A na B, Chikunji, Mtope, Likunja, Nkowe, Nandagala, Namichiga na Mandawa.”