Makonda asema ujenzi barabara ya Kivule-Kitunda bado unasuasua

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda ametaka umakini katika utoaji wa tenda za ujenzi wa miradi mbalimbali ili kuepuka dosari.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda ametaka umakini katika utoaji wa tenda za ujenzi wa miradi mbalimbali ili kuepuka dosari.

Amesema baadhi ya Makandarasi wanaopewa miradi wanashindwa kuikamilisha kwa wakati kutokana na kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na madeni.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Novemba 2, 2019 katika ziara ya kukagua miradi minne ya ujenzi, ikiwemo ujenzi wa barabara ya Kivule- Kitunda.

Makonda amesema Mkandarasi anayejenga barabara hiyo ambaye ni kampuni ya Nyanza bado anasuasua licha ya hivi karibuni kuagiza akamatwe na polisi.

Kutokana na hali hiyo ameagiza  Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kutompa tenda.

“Huyu mkandarasi huu uwe mradi wake wa mwisho katika Jiji la Dar es Salaam. Kama mnakumbuka hata Temeke aliwahi kufanya uzembe wa namna hii, vifaa hana vya kutosha kazi yenyewe haieleweki, tunataka Makandarasi wenye kasi kutekeleza miradi ya maendeleo,” amesem Makonda.

Amesema baadhi ya Makandarasi wanapewa tenda na kuishia kulipa madeni yanayowakabili kutokana na fedha wanazoingiziwa kukatwa na kusababisha miradi kutokamilika kwa wakati.

“Mnapotoa hizi tenda mjiridhishe wengine ndio kama hawa ambao hadi leo kazi hazionekani,  pia msiwape kazi kwa rushwa mtashindwa kusimamia miradi hii muhimu kwa wananchi,” amesema Makonda.

Miradi mingine aliyotembelea ni  ule wa mto Ng’ombe uliopo Sinza, ujenzi wa machinjio  ya Vingunguti pamoja na ujenzi wa soko la Tandale.

“Miradi yote inakwenda vizuri, shida ni huu wa Kivule yaani pamoja na kuwakamata lakini bado, huu wa mto Ng’ombe tutaendelea kufuatilia japo nimeridhishwa na utendaji wao,” amesema Makonda.

Mkandarasi anayesimamia ujenzi wa machinjio ya Vingunguti Eliasante Ulomi amesema Desemba 30, 2019 watakamilisha ujenzi.