Makonda kuchangisha Sh1 bilioni matibabu ya moyo kwa watoto - VIDEO

Wednesday September 18 2019

Dar es Salaam. Kiasi cha Sh1 bilioni kimetajwa kuwa kitakusanywa kwa njia ya changizo ifikapo Desemba 2019 kupitia benki, kampuni na watu binafsi kwa lengo la kusaidia zaidi ya watoto 500 wanaosubiri tiba ya upasuaji katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) nchini Tanzania.

Akizungumza leo Jumatano Septemba 18, 2019 wakati Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizindua kambi ya upasuaji wa moyo iliyoandaliwa na taasisi ya Shajjah Charity Group kutoka Nchi za Falme za Kiarabu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema fedha hizo zitakusanywa kuanzia Novemba 2019.

“Novemba hadi Desemba utakuwa ni mwezi wa shukrani kwa wananchi wa Dar es Salaam, huwa tunakuwa na tabia ya kutumiana kadi na shampeni kwa ajili ya mwaka mpya, ninakamilisha kamati na timu nzima kwa pamoja kwaajili ya kuchangisha Sh1 bilioni kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye maradhi ya moyo ili wafanyiwe upasuaji.”

“Ni rahisi mathalani benki zipo nyingi, tukitafuta kila benki ikatoa Sh20 milioni tu na tukaenda katika kampuni za magari ya malori 10 kila moja itoe Sh20 milioni, mategemeo yetu ni kwamba tukipata kampuni 50 na wananchi kile kipindi cha kwenda kuufunga mwaka 2019 kwenda kufurahia mwaka mpya… basi furahi na mtoto wa masikini aliyerejeshewa uhai wake kupitia wewe Mtanzania uliyeamua kutoa,” amesema Makonda.

Amesema licha ya hilo wamepanga pia kutoa bima za afya kwa watoto 100, “Kwa sababu lazima watahudhuria kliniki baada ya upasuaji nilimweleza Balozi wa Falme za Kiarabu nchini Tanzania, Khalifa Abdulrahman Mohamed Marzooqi na akaliunga mkono.”

Waziri Mwalimu amempongeza Makonda kwa kuja na wazo hilo huku akimtaka kuweka nguvu zaidi kuisogeza mbele sekta ya afya katika mkoa wa Dar es Salaam.

Advertisement

“Kwa ajili ya matibabu ya watoto ni jambo kubwa, lakini pia amesema atachangia bima kwa watoto 500, kupata Sh1 bilioni.”

“Ninarudia kusisitiza sisi kama Serikali tutaendelea kutimiza wajibu wetu wa kuweka fedha, hivi karibuni tumewekeza Sh150 milioni hapa JKCI za uendeshaji tutalipa mishahara fedha za maendeleo pamoja na uwezeshaji nitumie fursa hii kuwashukuru sana kwa ujuzi unaotolewa kwa wataalamu wetu,” amesema Mwalimu.

Advertisement