Mbunge aliyesema wahudumu ATCL hawana mvuto aomba msamaha

Thursday November 14 2019

Mbunge wa Kigoma Kusini nchini Tanzania (CCM)

Mbunge wa Kigoma Kusini nchini Tanzania (CCM) Husna Mwilima 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Kigoma Kusini (CCM), Husna Mwilima ameomba radhi kwa kauli aliyoitoa bungeni kuwa wahudumu wa ndege wanaoajiriwa na Shirika la Ndege nchini (ATCL) hawana mvuto kwa wateja.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 14, 2019 bungeni mjini Dodoma kabla ya kuuliza swali la nyongeza.

Novemba 7, 2019 mbunge huyo alisema wahudumu hao hawana mvuto kwa wateja wakati akichangia Mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo.

Amesema siku hiyo wakati akichangia alitoa kauli iliyowagusa Watanzania na baadhi ya wabunge.

“Nilifanya hivyo kwa kutaka kuboresha shirika letu la ATCL lakini kwakuwa inawezekana kwa namna moja ama nyingine nikawa nimewakwaza Watanzania wenzangu hasa wanawake naomba nichukue nafasi hii mheshimiwa spika kuomba radhi kwa kauli yangu niliyoitoa bungeni,” amesema.

Baada ya kuomba msamaha, Spika Job Ndugai amesema kitendo kilichofanywa na mbunge huyo ni cha kiungwana.

Advertisement

Wakati akichangia Novemba 7, 2019 Husna alisema, “mheshimiwa waziri mimi nataka nitanie kidogo hizi ndege zetu zinafanya vizuri sana lakini mle ndani hebu tuangalie tunaowaajiri. Wale maair hostess (wahudumu) hata ukimuita mle ndani akigeuka abiria anaona kweli tuna maair hostess mle ndani.”

“Sijui mnatumia vigezo gani? Unakuta air hostess mfupi, hana mvuto wa kuifanya ndege zetu zionekane. Leo mimi hapa nimezeeka na miaka 50 na ukiniweka…”alisema kabla ya kukatishwa na utaratibu uliombwa na Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma.

Musukuma alisema huo ni ubaguzi na kwamba kuna wengine wanazaa watoto ambao hawana maumbo kama anayoyasema mbunge huyo.

Mbunge huyo alisema sifa ya mhudumu wa ndege ni lazima awe mrefu na amenyooka akiwa mwanaume ama mwanamke na kuomba jambo hilo lizingatiwe.

Hata hivyo, ATCL ilijibu suala hilo kwa mkurugenzi mtendaji wake, Ladislaus Matindi kusema hawaajiri wahudumu kwa ajili ya kuuza sura.

 

Advertisement