Mchungaji Msigwa awazungumzia Kubenea, Komu

Muktasari:

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amewatuhumu wabunge wa chama hicho, Saed Kubenea na Anthony Komu kuwa wanafanya siasa kuhakikisha anashindwa katika uchaguzi wa uenyekiti wa Kanda ya Nyasa.

Mbeya. Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa amewatuhumu wabunge wa chama hicho, Saed Kubenea na Anthony Komu kuwa wanafanya siasa kuhakikisha anashindwa katika uchaguzi wa uenyekiti wa Kanda ya Nyasa.

Mchungaji Msigwa amekwenda mbali zaidi na kubainisha kuwa wabunge hao wanataka ashindwe kwenye uchaguzi huo ili iwe rahisi kwao kupanga mikakati kuhakikisha mwenyekiti wa wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe anashindwa katika uchaguzi utakaofanyika Desemba 18, 2019.

Siku za hivi karibuni sauti zinazodaiwa kufanana na Kubenea (Ubungo) na Komu (Moshi Vijijini) zimesambaa katika mitandao ya kijamii, wakisikika wakizungumzia chaguzi ndani ya chama hicho na jinsi ya kuwaangusha baadhi ya wagombea.

Mchungaji Msigwa aliyeandika andiko refu lenye kichwa cha habari  ‘Nimesamehe, lakini Komu na Kubenea wanatafuta nini Upinzani’, kuliweka mtandaoni amehoji wabunge hao wanatafuna nini upinzani.

“Leo ni siku ya tatu tangu pasikike sauti za mazungumzo baina ya watu watatu. Kwa wawili inatokea kwa mara ya pili sasa Mungu anawaanika kwa uovu wao, uasi wao na utovu wao wa nidhamu kwa Chadema na upinzani mzima kwa ujumla. Hawa ni Komu, Kubenea na kiongozi mmoja kutoka mkoani Mbeya.”

“Kimsingi mazungumzo hayo yaliyozagaa katika mitandao ya kijamii nchini kote, yalikuwa yakinilenga mimi mwenyewe binafsi lakini pia hatima yake ikiwa inamlenga zaidi Mbowe,” amesema Mchungaji Msigwa.

Ameongeza, “Kubenea na Komu walikuwa wanatoa maelekezo kwa kiongozi huyo wa Mbeya kuwa wahakikishe mimi (Msigwa) siwi mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini katika uchaguzi ujao wakiamini pia kuwa kunikwamisha kwao kutasaidia pia kutimiza adhima yao ya kutaka Mbowe naye ang'oke katika nafasi hiyo katika uchaguzi ujao wa kitaifa ulio karibia sana.”

Amesema si mbaya kwa mtu kutaka kiongozi fulani ang’oke kwa kuwa ndio demokrasia lakini anashangazwa na Kubenea na Komu kuvuka mipaka ya misingi ya kidemokrasia, umoja na mshikamano.

“Wamesikika wakizungumza namna ya kutafuta wagombea wenzangu na kuwataka waunganishe nguvu na namna ya kutumia pesa wajumbe (wapiga kura) kuwahonga wasinichague na mengine mengi.”

“Kwa macho ya kawaida unaweza ukadhani ni jambo la kawaida sana. Unaweza ukadhani ndiyo ushindani wenyewe wa kidemokrasia. Lakini ukweli kwa mujibu wa katiba ya Chadema walichofanya ni makosa makubwa sana,” amesema Msigwa huku akitaja makosa hayokuwa ni kufanya kampeni kabla ya wakati, kubariki rushwa  na kuchochea makundi.

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la kesho Jumatato Novemba 27, 2019