VIDEO: Mgombea ubunge Chadema aomba kulala rumande, polisi wamkamata

Mgombea ubunge Chadema aomba kulala rumande, polisi wamkamata

Muktasari:

Mgombea ubunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Chief Kalumuna amesema hana imani na usalama wake akienda nyumbani kwake bila kuapishwa kwani kwa mazingira, hali ya kisiasa na joto la uchaguzi jimboni humo, lolote linaweza kumtokea na hivyo kushindwa kuapishwa kesho Alhamisi Oktoba 22, 2020 kama msimamizi wa uchaguzi alivyopanga.

Bukuba.  Polisi mkoani Kagera wanamshikilia mgombea ubunge wa Bukoba mjini (Chadema), Chief Kalumuna baada ya kutokea mvutano kati yake na msimamizi wa uchaguzi kuhusu utaratibu wa kuapishwa kumwezesha kuingia kwenye vituo vya kupigia kura na kituo cha majumuisho.

Kabla ya kumtia mbaroni mgombea huyo, polisi walilazimika kufyatua mabomu kadhaa ya machozi baada ya wafuasi wa mgombea huyo kufunga milango ya uwanja wa Kaitaba  ambako shughuli ya kuapisha mawakala ilikuwa ikifanyika.

Awali, Kalumuna alimwomba Mkuu wa Polisi Wilaya ya Bukoba kumhifadhi katika  mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi mjini Bukoba hadi kesho Alhamisi saa 4:00 asubuhi atakapoenda kuapishwa.

"Kwa sababu kisheria wagombea na mawakala wanapaswa kuapishwa leo Oktoba 21, 2020 ambayo ni siku saba kabla ya siku ya uchaguzi; basi OCD nakuomba nipande karandika lako ili ukanihifadhi mahabusu hadi kesho saa 4:00 asubuhi utakaponipeleka kuapishwa. Ukifanya hivyo utanisaidia sana kwa ajili ya usalama wangu," Kalumuna amesema.

Akifafanua ombi lake hilo, mgombea huyo amesema hana imani na usalama wake akienda nyumbani kwake bila kuapishwa kwani kwa mazingira, hali ya kisiasa na joto la uchaguzi jimboni humo, lolote linaweza kumtokea na hivyo kushindwa kuapishwa Oktoba 22, 2020 kama msimamizi wa uchaguzi alivyopanga.

Kalumuna amefikia hatua ya kuomba kwenda kulala mahabusu baada ya ombi lake la kumtaka msimamizi wa uchaguzi jimbo la Bukoba mjini, Mourice Limbe  kumpa taarifa ya maandishi kuwa wagombea ubunge na madiwani wataapishwa Oktoba 22, 2020 badala ya Oktoba 21, 2020 inavyoelekezwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi.

Licha ya kuwaapisha mawakala wa vyama vyote, msimamizi wa uchaguzi aliwatangazia wagombea udiwani na ubunge waliokuwepo eneo hilo kuwa wao wangeapishwa kesho Oktoba 22, 2020.