Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mnyukano hadharani wa wateule wa Rais kitendawili

Dar es Salaam. Ni jambo la kawaida kwa viongozi kuwa na kauli moja hadharani, lakini kauli zinazotofautiana wateule wa Rais katika suala moja, zinaibua maswali katika dhana ya uwajibikaji wa pamoja.

Katika dhana hiyo, viongozi hutakiwa kuwa na kauli moja kuhusu tukio au msimamo wa jambo fulani hata kama kwenye vikao vya ndani wanatofautiana, hii ni kwa sababu ya kutotaka kuwayumbisha wananchi.

Uwajibikaji huo wa pamoja ulitarajia katika suala la utata wa mshindi wa mashindano ya Big Brother 2014, Idris Sultan.

Nyota huyo wa mitandao ya kijamii alituma picha inayoonyesha sura yake ikiwa imewekwa kwenye mwili uliokalia kiti chenye nembo ya Serikali na kichwa kingine chenye sura ya Rais John Magufuli, ikiwa kwenye mwili uliovaa shati jeupe na suruali yenye mikanda maarufu ya cross belt au suspenda.

Na chini ya picha hizo kukiwa na ujumbe unaomshauri Rais kuwa “kwa siku moja tukabadilishana kazi ili a-enjoy siku yake ya kuzaliwa kwa amani”.

Lakini mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akamuamuru Idris aripoti polisi kutokana na kitendo hicho.

“Naona mipaka ya kazi yako huijui, nenda sasa hivi kituo chochote cha polisi uwaambie Makonda kaniambia nije utakuta ujumbe wako,” aliandika Makonda, akitoa amri kwenye mitandao ya kijamii.

Na huo ukawa mwanzo wa Makonda kutofautiana na wateule wenzake wa Rais-- Dk Hamisi Kigwangalla (Waziri wa Maliasili na Utalii) na Jokate Mwegelo (mkuu wa wilaya ya Kisarawe ambaye hajaonyesha waziwazi kuingia katika sakata hilo)-- huku mkuu wa mkoa wa Iringa, Ali Hapi akimuunga mkono mkuu huyo wa Dar es Salaam.

“Nimeambiwa kuna msanii wa vichekesho anatafutwa na polisi. Mniambie nitajitolea mwanasheria wa kwenda kumuwekea dhamana na kumtetea,” aliandika Dk Kigwangalla katika akaunti yake ya Twitter.

“Rais wetu ni mtu wa watu na imejidhihirisha kwa jinsi wananchi walivyojitolea kumuombea dua siku ya kuzaliwa kwake. Wameonyesha upendo.”

Mkuu wa mkoa anaagiza raia aripoti polisi, waziri anataka taarifa za tukio ili atafute mwanasheria wa kumsaidia mtu huyo.

Inakuwaje watendaji ambao wanateuliwa na mtu mmoja kupishana na kutokuwa na uwajibikaji wa pamoja? Ndivyo wengi wanavyohoji.

Katibu mkuu mstaafu wa Utumishi, Ruth Mollel anasema hizo ni dalili za kukosa mafunzo ya uongozi na kutowasiliana.

Mollel alisema watendaji na watumishi Serikali walikuwa wakipewa mafunzo vyuoni kati ya wiki mbili hadi miezi mitatu, jambo lililowasaidia katika utendaji wao wa kazi.

“Kwa maoni yangu inaelekea hawa watu hawajapata mafunzo ya uongozi. Zamani ukiteuliwa kuwa kiongozi, ulipelekwa Mzumbe (chuoni) kusoma miezi mitatu. Hata madaktari walipelekwa kufundishwa utawala. Utumishi wa umma walikuwa wanapelekwa mafunzo ya wiki mbili.

“Inaelekea kama hakuna mawasiliano kwa sababu kama Makonda ametamka yale, mwenzake badala ya kujibu mtandaoni angeweza kuwasiliana naye tu.”

Mollel, ambaye ni mbunge wa viti maalumu Chadema, alisema kulumbana kwa wateule wengi wa Rais hakuonyeshi umoja wa Serikali na kunavunja moyo watu wa kawaida.

“Tunajiuliza inakuwaje wateule wa rais wanapishana wakati wangeweza kukaa wenyewe na kumaliza mambo husika,” alisema.

Wakati Kigwangalla akionyesha kutofautiana na kitendo cha Makonda, mkoani Iringa Hapi alimtetea gavana huyo wa Dar es Salaam.

“Ningeshangaa sana kama mtu aliyemdhihaki Rais wa nchi yetu, angeachwa bila kuchukuliwa hatua za kisheria. Hongera Makonda,” ameandika Hapi katika ukurasa wake wa mitandao ya kijamii.

Lakini mkuu wa wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo hakutaka kuonyesha kama anashabikia wala kupinga tukio hilo katika ukurasa wake wa Twitter, badala yake akatoa ujumbe unaoweza kuwafanya wafuasi wake watafsiri kuwa amezungumzia sakata hilo.

“Inawezekana ukawa una nguvu ya kufanya jambo fulani lakini haimaanisha utumie nguvu uliyonao kulifanya,” ameandika mshiriki huyo wa Miss Tanzania mwaka 2006.

“Ndio maana tuombe Mungu tutanguliwe zaidi na busara na hekima katika maamuzi kukwepa kuumiza watu bila sababu za msingi. Ijumaa Kareem.”

Tafsiri ya ujumbe wa Jokate inatokana na tukio hilo kumuhusisha mtu mwenye nguvu zote za dola na mamlaka katika ngazi ya mkoa, yaani Makonda dhidi ya mwananchi wa kawaida, yaani Idris.

Siku ya kwanza aliporipoti kituo kikuu cha polisi mkoani Dar es Salaam, Idris, ambaye ni mchekeshaji, alihojiwa na kisha kupekuliwa nyumbani kwake ambako polisi walichukua kompyuta yake ya mpakato na jana walichukua simu zake.

Baada ya mkuu huyo wa mkoa kueleza hayo, Dk Kigwangalla alishindwa kuvumilia badala yake akaandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram,

Si mara ya kwanza kwa watendaji wa Serikali kulumbana mitandaoni kwani Kigwangalla aliwahi kulumbana na aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba kuhusu mradi wa kupandisha watalii Mlima Kilimanjaro kwa kutumia viberenge.

Rais Magufuli amekuwa akikemea na kuchukua hatua kwa wateule ambao wanagombana katika utendaji wao, hasa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wao.

Wanasheria wanena

Wakizungumzia suala la Idris kuitwa polisi, wanasheria wamesema wana imani msanii huyo hakutumia picha kwa nia ovu.

Wamesema mtu anapotumia picha ya mtu mwingine anakuwa na kosa pale anapoitumia nia ovu. Baadhi walisema Idris ni mchekeshaji hivyo suala hilo lilipaswa kuzingatiwa kabla ya hatua zaidi.

Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema matumizi ya picha ya Rais kwa nia ya kuchekesha hutegemea na jinsi ilivyotumiwa. “Ni jambo ambalo si sahihi lakini inapaswa tu kumuonya,” alisema Kyauke.

Alitoa mfano wa Baraka Mwakipesile, maarufu kama Baraka Magufuli anayeigiza sauti ya Rais akisema anachokifanya hakina tofauti sana na anayebadilisha picha yake na Rais bila matumizi yoyote mabaya.

“Kama mtu ametumia picha ya Rais bila kuvunja maadili wala kuitumia vibaya, kijamii na kisheria kosa lake si jinai ni la kuonywa tu,” alisema Dk Kyauke.

Makamu wa rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi alisema inapaswa kuangaliwa mazingira ya kazi ya mtu kabla ya kumshtaki.