Msanii Harmonize asimulia alivyouza nyumba tatu kuwalipa Wasafi Sh500 milioni

Muktasari:

Msanii Abdul Rajabu maarufu Harmonize amesema aliuza nyumba zake tatu na baadhi ya mali ili kuilipa lebo ya Wasafi Sh500 milioni kwa ajili ya kupata  hakimiliki ya kutumia nyimbo zake na jina.


Dar es Salaam. Msanii Rajabu Abdul  maarufu Harmonize amesema aliuza nyumba zake tatu na baadhi ya mali ili kuilipa lebo ya Wasafi Sh500 milioni kwa ajili ya kupata  hakimiliki ya kutumia nyimbo zake na jina.

Harmonize ameeleza hayo leo Alhamisi Oktoba 24, 2019 katika kipindi cha XXL cha Redio Clouds.

Amebainisha kuwa mkataba alioingia na lebo ya Wasafi inayomilikiwa na msanii Diamond Platnumz ilikuwa na kipengele cha kulipa kiasi hicho cha fedha ikiwa atavunja mkataba ili aweze kuendelea kutumia nyimbo pamoja na jina lake la kisanii.

“Mkataba ulinitaka nilipe Sh500 milioni na gharama za kuandaa nyimbo zangu zote wakati nikiwa chini ya Wasafi,” amesema Harmonize.

Amebainisha kuwa alifanikiwa kulipa kiasi kikubwa cha fedha hizo  jambo lililomuwezesha kuendelea kutumia nyimbo zake na jina.

Akizungumzia uhusiano wake na lebo ya Wasafi, Harmonize amesema si mzuri kama zamani, “licha ya kuwa niliondoka baada ya kupata baraka zote kutoka kwa uongozi wa Wasafi.”

Amefafanua kuwa kulikuwa na tatizo ambalo walishindwa kulimaliza alipokuwa katika lebo hiyo na aliamua kujitoa.

“Bado naamini mimi ni familia ya Wasafi na ninawaheshimu sana. Nilitoka si kwa ubaya na wala ugomvi. Nilikaa na uongozi na kuomba ridhaa yao nifanye muziki wangu mwenyewe baada ya kuona tumeshindwa kumaliza mambo yetu,” amesema.