Msomi azungumzia sababu za kina Nape kuomba radhi

Wednesday September 11 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana amefafanua sababu ya wabunge wa chama tawala cha CCM waliojitokeza kumwomba msamaha Rais John Magufuli akisema ni kuonyesha dhamira ya dhati.

Mbali na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye aliyekwenda Ikulu ya Dar es Salaam jana Jumanne Septemba 10, 2019 kuomba msamaha, wengine ni January Makamba (Bumbuli) na William Ngeleja (Sengerema) ambao Rais Magufuli alisema amewasamehe.

Akizungumza kwa simu na Mwananchi leo Jumatano Septemba 11,2019, Dk Bana amesema kitendo hicho kimethibitisha kuwa Rais Magufuli hupenda uwazi na ukweli.

“Kama umemfuatilia Rais wetu, hataki vitu vya kufichaficha, anapenda uwazi na ukweli. Kitendo cha kuomba msamaha na hasa ukiomba hadharani ni jambo jema. Kwa sisi waumini dini mbalimbali ni sahihi,” alisema Dk Bana.

Kuhusu maombi hayo ya msamaha, Dk Bana alisema, “Wamepima uzito kauli walizotoa za kebehi za kejeli kwa mheshimiwa Rais mwenye dhamana ya kuongoza taifa letu na vilevile wakaomba ushauri, nina imani wameshauriwa wakachukua jukumu wao wenyewe wakaenda kuomba msamaha.”

Amesema kitendo cha kuomba radhi ni cha kiungwana na kukomaa kisiasa hasa mwanasiasa anapoona ametoka nje ya mstari.

Advertisement

“Kitendo cha kukomaa cha kumwangukia Rais ni kitendo cha busara, kwa sababu bado ni vijana, bado wana matazamio mbalimbali. Kosa siyo kutenda kosa, ila kurudia kosa,” amesema.

Licha ya kukubali kuwa wanasiasa hao walikwazwa, lakini amesema kama viongozi walipaswa kuonyesha ukomavu kwa kuwa ukubwa ni jalala.

Advertisement