Mtanzania apata mabilioni, auza mfumo wa kununua gesi kadiri unavyotumia

Friday January 17 2020

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Safaricom,

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Safaricom, Michael Joseph (katikati) na Alok Sharma mwakilishi kutoka Shirika la Mendeleo la Uingereza wakionyesha mita ya gesi ya majumbani wakati halfa ya mauziano ya tekilojia hiyo iliyofanyika Nairobi nchini Kenya. Kushoto ni mbunifu wa mita hiyo, Andron Mendes. Na Mpigapicha Maalum 

By Gadiosa Lamtey, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mtanzania, Andron Mendes ameuza mfumo wa mita ya kulipia gesi ya kupikia kadiri unavyotumia (PAYG) kwa kampuni ya Circle Gas ya Uingereza kwa Sh57.6 bilioni ili usambazwe kwa nchi nyingine za Afrika.

Mgunduzi huyo alisema amefikia uamuzi huo baada ya kuona kuwa kuendesha mradi huo kutahitaji mtaji mkubwa ili kuwafikia idadi kubwa ya Watanzania huku mahitaji yake yakiongezeka.

Jumatatu ya wiki hii, kampuni hiyo ya Uingereza ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikieleza kufikia makubaliano ya kuichukua teknolojia ya kampuni ya Kopagas inayomilikiwa na Mtanzania huyo kwa Dola 25 milioni (Sh bilioni 57.6)

Ununuzi huo utaiwezesha Circle Gas kupata teknolojia ya PAYG.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watu wapatao milioni 900 sawa na asilimia 70 ya watu wa Kusini mwa Jangwa la Sahara bado hawajaungwa kwenye mfumo wa teknolojia ya gesi safi ya kupikia.

Wagunduzi hao watabaki kuwa watendaji wakuu wa mradi huo mpya.

Advertisement

Circle Gas yenyewe itakuwa ikitoa nishati ya gesi kwa soko kubwa kwa kuinua ugunduzi wa teknolojia hiyo ulioanzishwa na Kopagas ili kuhakikisha soko lake linapenya Afrika Mashariki.

Akizungumza na gazeti la The Citizen ambalo ni gazeti dada la Mwananchi, Mendes alisema, “Hakuna sababu ya kushikilia teknolojia ambayo inapunguza matumizi ya mkaa kwa sababu tu umeigundua. Nimeamua kuiuza teknolojia hiyo kwa watu wenye fedha ili waisambaze Afrika.

Alisema kwamba mchakato wa kuiuza ulianza tangu mwaka jana na kufikia mwaka huu wamekamilisha, akiongeza kuwa Tanzania ina vipaji vingi vinavyohitaji kukuzwa akiwataka vijana kujiamini.

Aliongeza kuwa Sh57.6 bilioni ni kwa ajili ya kurudisha mtaji wa kuwekeza na kuuzia teknolojia.

“Katika kampuni hii mpya tutamiliki asilimia 15 na nikiongeza wafanyakazi wangu tutahamia kwenye kampuni mpya kwa hiyo hatutapoteza kazi,” aliongeza Mendes.

Alisema alipata wazo hilo mwaka 2012 na kuanza kuliendeleza na kukuza teknolojia hiyo kwa miaka saba. Suluhisho la upatikanaji wa gesi safi ya kupikia kwa wananchi wenye kipato cha chini utawawezesha kupunguza matumizi ya mkaa.

Tangu alipoanza mradi huo Mei 2016, jumla ya watu 1,430 wa jijini Dar es Salaam wameshaunganishwa akisema walikuwa na mpango wa kuunganisha wateja 200,000 kufikia mwaka 2021 lakini kutokana na ufinyu wa mtaji wameamua kuiuza teknolojia hiyo kwa Circle Gas .

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Circle Gas, Volker Schultz alisema kwamba watashirikiana na KopaGas na Kampuni ya simu za mkononi ya Kenya, Safaricom ili kuunganisha nguvu na kubadilishana uzoefu kwa ajili ya kuleta upatikanaji wa gesi ya bei nafuu kwa mamilioni ya watu katika bara la Afrika.

Kwa upande wake Ofisa Mkuu wa Safaricom, Michael Joseph alisema, “Hii ni fursa nyingine muhimu kwa kampuni yetu kushiriki katika mradi huu utakaobadilisha maisha ya watu na kuthibitisha umuhimu wa teknolojia katika maisha ya kila siku.

Alitolea mfano mfumo wa utumaji fedha kwa kutumia simu za mkononi yaani M-Pesa na mtandao wa GSM ulivyotumika kubadilisha maisha ya watu.

Advertisement