Mtei: Viatu vya Mwalimu havijamtosha kiongozi yeyote

Friday October 11 2019

 

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Arusha. Waziri wa zamani wa fedha katika Serikali ya Awamu ya Kwanza, Edwin Mtei amesema tangu kiongozi huyo afariki dunia miaka 20 iliyopita, hakuna kiongozi yeyote aliyeweza kuvaa viatu vyake na vikamtosha.

“Hakuna ninayeweza kumfananisha na hayati Baba wa Taifa, amefanya mambo makubwa kwa Taifa hili,” alisema Mtei ambaye alishika nafasi hiyo ya uwaziri wa fedha kwa miaka miwili 1977-79.

“Aliwaunganisha Watanzania, kuweka misingi imara ya amani na utulivu, pia kuanzisha mapinduzi makubwa ya kidemokrasia na kiuchumi.”

Mtei, ambaye alikuwa gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) 1966-1974, alifanya mahojiano maalumu na Mwananchi kuhusu miaka 20 tangu kifo cha Mwalimu Nyerere.

Mwalimu alifariki dunia Oktoba 14, 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London, Uingereza na alizikwa Butiama mkoani Mara. Oktoba 14 itakuwa ni miaka 20 tangu kifo chake.

Mtei, ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC), alisema Mwalimu pia alikuwa rafiki yake.

Advertisement

Alisema wakati Taifa liko kwenye kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, kuna mambo mengi muhimu ambayo Watanzania, hasa vijana, hawayafahamu vizuri na viatu vyake vimekosa mtu wa kuvivaa na kumtosha.

Mtei aliyepata shahada ya kwanza katika Chuo Kikuu cha Makerere, Uganda mwaka 1957, alisema Mwalimu alikuwa mzalendo wa kweli, aliyeipenda Tanzania kuliko kitu kingine na mchango wake kwa Taifa hautasahaulika.

Alisema historia ya Taifa hili haiwezi kuandikwa vyema bila kutaja mchango wa Mwalimu katika kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja, kuweka misingi imara ya utaifa, umoja na mshikamano ambao utabaki kuwa wa mfano duniani.

Ujenzi wa demokrasia

Mtei, ambaye aliiasisi Chadema Mei 1992, alisema Mwalimu alikuwa mwana demokrasia halisi na aliweza kujenga vyema demokrasia ili kuhakikisha Watanzania wanakuwa na fursa sawa, kushiriki katika ujenzi wa taifa lao, kushiriki katika siasa na kutoa maoni.

Nyerere ndiye alikubali mfumo wa vyama vingi licha ya asilimia 80 ya Watanzania kupendelea mfumo wa chama kimoja wakati huo.

“Wakati wa kuanza mfumo wa vyama vingi Nyerere angeweza kupinga kwani kura za maoni zilionyesha Watanzania wengi walikuwa hawajajiandaa, lakini kwa kuwa alikuwa ni mpenzi wa demokrasia na mwenye maono ya mbali, aliungana na wachache kutaka Tanzania kuingia katika mfumo wa vyama vingi,” alisema Mtei.

Alisema Mwalimu alikuwa anafurahi kuona siasa za Tanzania zinaimarika kwa kutoa fursa ya sera mbadala kama ambazo Chadema walikuja nazo.

“Mwalimu alipenda mabadiliko, alitaka kila wakati kuwepo na sera mbadala ili kushindanisha vyama na ndio sababu mimi nilianzisha Chadema na hakuwahi kunipinga japo alikuwa mtu wangu wa karibu,” alisema Mtei ambaye Julai 12, alifikisha miaka 87.

Alisema katika maisha yake, Mwalimu hakuwahi kuwabagua watu kwa vyama vyao, ama tofauti za mitazamo ya kisiasa na alipenda CCM ifanye siasa za ushindani ili kujiimarisha.

Alifafanua kuwa katika masuala ya maendeleo na kujenga uchumi, Mwalimu aliweka misingi imara ambayo hadi leo inaendelezwa.

“Mwalimu Nyerere alihakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote bila kujali, makabila yao, dini wala rangi,” alisema.

Aliusifu uongozi wa Mwalimu kuwa ulisababisha fursa za kiuchumi kwa wote na ndio sababu Watanzania waliunganishwa kwa pamoja bila kujali tofauti zao.

“Mwalimu alikuwa na ndoto za ukombozi wa Watanzania wote, ndio sababu alikuwa na sera mbalimbali za kuwaunganisha kukaa pamoja na kufanya shughuli za kiuchumi,” alisema.

Ulinzi na usalama wa Taifa

Mtei alisema Mwalimu aliamini kuwa ni wajibu wa Serikali kuwalinda raia wake wakati wote.

“Mwalimu alikuwa hapendi Watanzania kupata shida za kiusalama hata raia wa kigeni hakupenda nao wapate tatizo la kiusalama, ndio sababu alikuwa anafikia hatua hadi kutoa majeshi kwenda kusaidia ulinzi na usalama katika mataifa mengine,” alisema Mtei.

“Wapigania uhuru wengi katika mataifa ya Afrika, waliishi Tanzania na Nyerere aliwahifadhi na kuwapa msaada wa kila hali ili wakitoka nchini waweze kurejesha umoja na mshikamano katika nchi zao,” alisema.

Sababu za kumuenzi Mwalimu

Mtei anasema Watanzania wanapaswa kuendelea kumuenzi Mwalimu katika mambo mengi mazuri ambayo ameyafanya.

“Watanzania tunapaswa kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuimarisha umoja wetu, bila kujali tofauti za kisiasa, rangi, dini wala makabila na huu ndio urithi mkubwa ambao Baba wa Taifa alituachia,” alisema.

Alisema pia vijana wengi hawamjui Mwalimu na wanakosa vitu vingi hivyo ni muhimu, wakapatiwa elimu ili kufahamu na kumuenzi na wenye uwezo waandike zaidi vitabu na kutoa machapisho hadi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Mwalimu Nyerere.

Uongozi wa Magufuli

Mtei anasema Rais John Magufuli anafanya kazi nzuri katika kuimarisha uchumi na anapaswa kuungwa mkono, lakini kuna mapungufu kuhusu masuala ya demokrasia na uhuru wa watu.

“Rais anafanya kazi nzuri sana, uchumi unakwenda, lakini pia amerejesha nidhamu serikalini na sasa watendaji wa serikali wanatoa huduma nzuri kwa wananchi,” alisema.

Alisema angependa Rais Magufuli, kuungwa mkono katika mambo mazuri ambayo anafanya ingawa bado hajafikia uwezo wa Baba wa Taifa.

Mtei alisema hata hivyo, Rais anapaswa kuwashirikisha watu wengi katika uendeshaji wa nchi, kwani kuna makundi mengine wakiwepo wapinzani wamewekwa nyuma jambo ambalo sio zuri.

Serikali ya mseto

Mtei alisema ili Watanzania wengi, wapate fursa ya kutoa mchango wao katika kuendeleza Taifa ni muhimu kuwepo mabadiliko ya Katiba ambayo yatawezesha kuundwa serikali ya mseto baada ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.

Anasema haiwezekani watu wanaungwa mkono na watu wengi, lakini baada tu ya uchaguzi wanakosa fursa ya kutoa mchango wao kwa maendeleo ya taifa.

“Mfano, Chadema tuna wafuasi wengi sana sio vizuri kuwaacha hivi hivi, baada ya uchaguzi ni muhimu wapate fursa kupitia muungano wa vyama kushiriki katika ujenzi wa taifa lao,” alisema.

Mtei alisema wakati Watanzania, wanamkumbuka Mwalimu ni muhimu pia kuendelea kushirikiana kwa pamoja kudumisha amani na utulivu katika taifa na kujitahidi kuondoa tofauti za kisiasa ili zisiwe chanzo cha vurugu.

Advertisement