Mwigulu: Nitashinda ubunge, wanaonibeza watageuka watazamaji

Wednesday April 15 2020

 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Homa ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 2020 ni kama imeanza kiaina bungeni baada ya Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM) Mwigulu Nchemba kujigamba kuwa tayari ameshashinda.

Akizungumza bungeni jana Jumanne Aprili 14, 2020, waziri huyo wa zamani wa mambo ya ndani amesema hana hofu na uchaguzi huo na wanaodhani hatashinda wasubiri 2021 watakapomuona tena bungeni.

Huenda ametoa kauli hiyo kutokana na mjadala unaoendelea mitandaoni na katika baadhi ya vyombo vya habari ikimtaja kigogo mmoja kulinyemelea jimbo hilo.

Jana wakati anachangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi katika wizara ya nchi ofisi ya Rais Tamisemi, sauti ya utani ilisika kutoka kwa mmoja wa wabunge upande wa upinzani wakimtaka Mwigulu ajiandae kupumzika.

“Kwa taarifa yenu mimi naweza kushinda ubunge katika jimbo lolote Tanzania na hasa katika majimbo yote ya upinzani, mimi nitashinda na mwakani mtaniona katika kiti hikihiki mtakapokuwa watazamaji kule juu,” amesema Mwigulu.

Kauli ya mbunge huyo imekuja wakati wabunge wengine wakiwa wametangaza kung’atuka nafasi zao pindi muda wao utakapokamilika.

Advertisement

Mwigulu ambaye amekuwa mbunge tangu 2010 amewataka wanaosema kuwa hatashinda ubunge wasahau kwani siasa hawazijui na kama wangezijua huenda wasingesema.

Hadi jana wabunge Anna Tibaijuka (Muleba Kusini) na Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) wametangaza kuwa hawatagombea tena ubunge katika uchaguzi mkuu ujao.

Advertisement