Nida yaeleza wenye ulemavu wa mikono watakavyosajili laini za simu

Friday December 6 2019

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, (Nida) nchini Tanzania, Arnold Kihaule 

By Baraka Samson, Mwananchi

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa, (Nida) nchini Tanzania, Arnold Kihaule amesema watu wenye ulemavu wa mikono hawataachwa nyuma katika usajili wa vitambulisho vya taifa na usajili wa laini za simu kwa alama za vidole.

Dk Kihaule amesema hayo leo Ijumaa Desemba 6, 2019 katika warsha ya siku moja iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa mawasiliano nchini humo.

Lengo la warsha hiyo kuwakutanisha watu mashuhuri wenye wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii, kampuni za simu nchini pamoja na wadau wa vyombo vya habari ili kutafuta mbinu ya kuhamasisha watu kuhakikisha wanasajili laini zako kwa alama za vidole kabla ya Desemba 31, 2019.

Akitoa ufafanuzi kuhusu watu wenye ulemavu wa viungo ambao nao wanataka kushiriki katika kujisajili, Dk Kihaule amesema katika usajili huo hakuna atakayeachwa nyuma hata wale ambao hawana mikono na wale ambao kutokana na shughuli zao za kazi, alama zao za vidole zimefutika wametafutiwa utaratibu mzuri ambapo wakifika katika ofisi husika za usajili watapewa maelekezo ya namna ya kujisajili.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Emmanuel Manasseh amesema dhumuni kuu la usajili kwa njia ya alama za vidole limelenga kuwalinda watumiaji wa simu dhidi ya matumizi mabaya ya mitandao, kuwatambua watumiaji  wa simu nchini na taarifa zao katika kampuni za simu husika, pia kuongeza  usalama katika matumizi ya simu na mitandao.

Mwakilishi wa kampuni za simu nchini Tanzania, Willliam Mpinga amesema katika usajili huo wa laini za simu kwa alama za vidole hadi sasa watu takribani milioni 18 wameshasajiliwa huku watu milioni 28 wakiwa bado hawajasajiliwa.

Advertisement

Mpinga amesema kwa kasi ilivyo sasa hadi kufikia Desemba 31, 2019 kuna uwezekano asilimia 60 ya watumiaji wa simu wakaathirika mawasiliano ya simu yatakapozimwa kwa watu wote wanaotumia laini za simu bila kujisajili kielektroniki.

Mpinga amehitimisha kwa kuwataka watu mashuhuri wenye wafuasi wengi hapa nchini kutumia akaunti zao za mitandao ya kijamii kuhamasisha watu wajisajili kwa alama za vidole na kuhakikisha hadi Desemba 31, 2019 watumiaji wote wa simu wawe wameshasajiliwa.

Advertisement