MIAKA 20 BILA YA NYERERE: Nyerere ataifisha majumba, mabenki na viwanda-10

Saturday October 12 2019

 

Siku chache baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, Serikali ilianza kutaifisha mali. Mabenki yote yaliyokuwa yakifanya kazi zake nchini, isipokuwa Benki ya Ushirika zilitaifishwa.

Henry Bienen katika kitabu chake, Tanzania: Party Transformation and Economic Development, anasema Februari 11, zikiwa ni juma moja tu baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, Serikali ilitangaza kuzitaifisha benki zote tisa zilizokuwa nchini. Kuanzia hapo Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ikaanzishwa na kisha ikawa benki pekee ya biashara nchini.

Benki pekee zilizoachwa bila kutaifishwa ni zile za Washirika (Co-operative Bank) pamoja na Benki ya Watu wa Zanzibar (Zanzibar People’s Bank). Ingawa Serikali ilionyesha nia ya kuendelea kufanya kazi na wafanyakazi wa hizo benki zilizotaifishwa, ilionekana kana kwamba walianzisha mgomo baridi.

Wafanyakazi wa benki tatu za Kiingereza—Standard, Barclays na National and Grindlays—ambao idadi yao ilikuwa ni 52 waliondolewa mara moja kutoka katika benki hizo ili wasiendelee kufanya kazi na benki mpya iliyoanzishwa.

Kwa mujibu wa James Mittelman katika kitabu chake, Contesting Global Order: Development, Global Governance, and Globalization, wafanyakazi hao 52 ni 25 wa Benki ya Standard, 16 wa Barclays na 11 wa National and Grindlays—zote za Uingereza.

Kwa kipindi chote cha miaka ya 1970, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) iliendelea kubaki kuwa benki pekee ya biashara katika Tanzania Bara. Jumanne ya Februari 14, zikiwa ni siku tisa tu baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, bunge lilipitisha muswada wa sheria ya kuanzishwa kwa NBC kuchukua nafasi ya benki zilizotaifishwa.

Advertisement

Benki zilizotaifishwa Februari 6 ni pamoja na Bank of Baroda (India), Bank of India, Barclays Bank, National & Grindlays Bank, Standard Bank na General Bank of the Nertherlands.

Hata hivyo, taasisi nyingine za kifedha zilianza kuibuka taratibu zikiwamo ‘Tanzania Investment Bank’ na ile iliyojulikana kama ‘Tanzania Rural Development Bank,’ ambayo mwaka 1984 ilikuja kubadilishwa jina na kuitwa CRDB na kufanya benki za biashara katika Tanzania kuwa mbili. Hiyo ni kwa mujibu wa kitabu ‘Tanzania at the Turn of the Century: Background Papers and Statistics kilichoandaliwa na Benno Ndulu na Charles K. Mutalemwa.

Siku chache baada ya kutaifishwa kwa mabenki, makampuni makubwa ya biashara nayo yalitaifishwa. Mengi ya hayo yalikuwa ya Waingereza. Hayo ni pamoja na Smith Mackenzie & Co. Ltd., Dlzety East Africa Ltd, International Trading & Credit Co. of Tanganyika Ltd, Cooperation Supply Association of Tanganyika Ltd, A. Bauman & Co. Ltd, Twentsche Overseas Trading Co., African Merchantile Co na Wigglesworth & Co.

Shirika la Bima la Taifa (The National Insurance Corporation) liliwekwa chini ya mamlaka ya umma na kupewa hodhi ya mambo yote ya bima nchini.

Kiasi cha makampuni manane ya usagishaji ambayo yalikuwapo wakati huo, nayo yalitaifishwa na Serikali kuwa mali ya umma na kisha kuwekwa chini ya Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC—National Milling Corporation).

Makampuni hayo ni pamoja na Tanzania Millers, Chande Industries, Pure Foods Products, G. R. Jibraj, Moor-Mohamed Jessa, Uyela Sathar Mills, Associated Trades Ltd na Rajwani Mills. Serikali ilinyakua asimilia 60 ya hisa katika viwanda kadhaa. Kwa mfano, Ijumaa ya Oktoba 27, 1967 serikali ilichukua asilimia 60 ya biashara ya mkonge na kuiundia Mamlaka ya Mkonge Tanzania.

Makampuni mengine ambayo serikali ilichukua asilimia kubwa ya hisa ni pamoja na Beer Breweries Ltd, Kilimanjaro Brewery, Tanzania Brewery, British American Tobacco Co, Bata Shoe Co, Tanganyika Metal Box Co, Tanganyika Extract Co na Tanganyika Portland Cement.

Alhamisi ya Aprili 22, 1971 Bunge la Tanzania lilipitisha muswada wa ‘Sheria ya Utaifishaji Majengo’ (Acquisition of Buildings Act, 1971) ambayo Rais aliisaini na kuwa sheria. Halafu mwezi huohuo Rais Nyerere akatangaza kuwa zaidi ya majengo 1,000 yametaifishwa na serikali yake chini ya sheria hiyo.

Katika ukurasa wa 226 wa kitabu chake, Race, Nation, and Citizenship in Postcolonial Africa: The Case of Tanzania, mwandishi Ronald Aminzade ameandika: “Sheria hii ilimpa Rais mamlaka ya kutaifisha jengo lolote ambalo gharama ya ujenzi wake wakati wa kulitaifisha ni zaidi ya 100,000/- (dola 14,000 za Marekani—kwa mwaka 1971) na ambalo jengo lote halikaliwi na mmiliki wake.”

Sheria ya kutaifisha majumba ya mwaka 1971, pia ilikuwa na kipengele cha kuwepo kwa Baraza la Rufaa (Appeals Committee) ambapo kwa wale walioona majumba yao yametaifishwa kinyume na vipengele vya sheria ile wapeleke malalamiko yao. Kwa utaratibu huu baadhi ya majumba yalirejeshwa kwa wamiliki wa awali na mengine kwa njia za kifisadi.

Baadaye, mwaka 1973 sheria ile pia iliweka Baraza la Huruma (Clemency Committee) na kazi yake ilikuwa kusikiliza maombi ya wamiliki wa awali waliokuwa wazee na familia zao au kutokuwa na njia nyingine ya kupata kipato isipokuwa kupitia nyumba hizo. Baada ya kusikiliza maombi hayo, Ofisi ya Msajili ilikuwa na mamlaka ya kuamua kurejeshwa majumba au sehemu ya majumba hayo. Kuna mengine yalirejeshwa kwa kifisadi pia.

Alhamisi ya Oktoba 5, 1972, Serikali ilitwaa usimamizi wa hoteli ya kifahari ya Kilimanjaro ya jijini Dar es Salaam kutoka kwa kampuni ya Israel ya Mlonot Ltd. Mkataba wa Mlonot ulikuwa umalizike mwaka 1975.

Alhamisi ya Februari 5, 1970 gazeti la The Standard nalo lilitaifishwa na serikali na kisha likabadilishwa jina na kuitwa Daily News. Awali The Standard lilikuwa linamilikiwa na kampuni ya Uingereza iliyoitwa Lonrho Limited. Mara baada ya kutaifisha gazeti hilo, mhariri mkuu akawa ni Rais Nyerere mwenyewe lakini mhariri mtendaji akawa ni Sammy Mdee.

Ijumaa ya Juni 2, 1978 Mwalimu Nyerere aliiamuru kampuni hiyo kufungasha virago na kuondoka nchini.

Tangu Uhuru mwaka 1961, kulikuwa na shule chache, na nyingi ya hizo zilikuwa chini ya taasisi za kidini—hususan kanisa na hasa Kanisa Katoliki. Kwa mfano, kwa mujibu wa kitabu The Pastor in a Changing Society cha Zawadi Job Kinyamagoha, mwaka 1968 Kanisa Katoliki lilikuwa na shule za msingi 1,378, nyingine 44 za sekondari, 10 za katekisti, vyuo nane vya walimu na shule 15 za biashara.

Chanzo hicho kinaungwa mkono na kitabu kingine cha David Westerlund kiitwacho Ujamaa na Dini: A Study of Some Aspects of Society and Religion in Tanzania, 1961-1977. Ili kuweka usawa katika elimu, Serikali iliamua kutaifisha shule zote.

Kwa mujibu wa kitabu Understanding World Christianity: Eastern Africa cha waandishi Paul Kollman na Cynthia Toms Smedley, hospitali nyingi, kama zilivyokuwa shule, ambazo zilianzishwa na Kanisa zilitaifishwa na serikali. Ukiacha zahanati nyingi na vituo vya afya zilizokuwa chini ya kanisa, kama Kanisa Katoliki, kulikuwa na hospitali kama Mtakatifu Joseph ya Perahimo ambayo ilianzishwa mwaka 1890 jijini Dar es Salaam na baadaye ikahamishwa katika karne ya 20. Nyingine ni Tosamaganga iliyoko Iringa na Mtakatifu Francis iliyoko Ifakara, ambayo ilianzishwa mwaka 1921 na pia Hospitali ya Bugando ya Mwanza iliyoanzishwa mwishoni mwa miaka ya 1960, pia Mtakatifu Francis ya Turiani.

Hata hivyo, kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1990, shule na hospitali nyingi zilizotaifishwa wakati wa Azimio la Arusha zilianza kurejeshwa kwa wamiliki wake wa awali.

Itaendelea kesho...

Advertisement