Polisi wamdaka mganga anayedaiwa kuwa chanzo cha mauaji ya wanawake 29

Muktasari:

Mganga wa kienyeji anayedaiwa kusababisha wanawake 29 kubakwa na kisha kuuawa baada ya kutoa masharti ya dawa kwa mtu aliyekua akitaka utajiri, amekamatwa na Polisi waliofanya oparesheni ya siku 11 maeneo ya Kanda ya Ziwa.

Geita. Jeshi la Polisi nchini, limewakamata watuhumiwa 504  wa makosa mbalimbali wakiwamo waganga wa jadi waliotoa dawa na masharti yaliyosababisha vifo vya wanawake 29  wa maeneo ya Kwimba, Misungwi na Shinyanga kuuawa kisha kubakwa ili muuaji apate  utajiri.

Mbali na mganga huyo, pia Polisi wanaishikilia fimbo ya mganga mmoja wa kienyeji iliyotumika kuwaaminisha wakata mapanga walioua askari wawili wa kituo cha polisi Nguruka mkoa wa Kigoma, askari mmoja wa Suma JKT na mgambo wa Mkoa wa Tabora, kisha kutolewa sehemu zao za siri kwa ajili ya dawa.

Akizungumza na waandishi wa habari  wakati akitoa tathmini ya opareshini maalumu ya kudhibiti matukio ya mauaji ya kupiga ramli chonganishi na makosa mengine kwa mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza na Shinyanga, Mkuu wa operesheni maalumu wa jeshi la Polisi, Mihayo Mskela leo Ijumaa Februari 14, 2020, inadaiwa fimbo hiyo ilitumika kuwakinga wakata mapanga na nguvu ya sheria pindi wanapokwenda kwenye matukio ya kihalifu ili wasikamatwe.

Katika operesheni hiyo iliyoanza Februari 3, 2020 hadi Februari 11, wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wa mauaji hayo ambao wapo wakata mapanga 44, watuhumiwa wa ramli chonganishi 75, kufanya uganga bila kibali, unyang’anyi wa kutumia silaha, kupatikana na nyara za Serikali, wizi wa mifugo na watuhumiwa wa makosa mengine.

Mskela amesema Mkoani Shinyanga wamekamatwa waganga wawili wa kienyeji ambao ni wakazi wa Idodomya, wanaodaiwa walikuwa wakiwaaminisha wauaji wa  wanawake 50 na kuwabaka watapata utajiri.

Amesema baada ya kuwakamata na  kuwahoji watuhumiwa hao waliwataja washirika wao wengine 17 ambao ni wakata mapanga na Polisi wanaoendelea kuwahoji.

Katika mkoa wa Kagera operesheni hiyo ilifanikiwa kuwakamata watu watano ambao walikuwa wakijihusisha na ukataji mapanga katika maeneo mbalimbali ya kanda ya ziwa.

Pia amesema Mkoani Tabora, wamemkamata mkazi mmoja wa Kitongoji cha Minala Sagida, kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi aliyetajwa kwa jina la Dotto Bundala (75) kwa kutumia nondo kwa lengo la kurithi mashamba yaliyoachwa na marehemu baba yake.