Rais Magufuli aridhishwa uchunguzi wa DNA, sampuli

Tuesday August 20 2019

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Jumanne Agosti 20, 2019 amemuagiza Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Profesa Ester Hellen Jason na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dk Fidelice Mafumiko kusimamia vizuri matumizi ya fedha zinatumika kununua mahitaji mbalimbali vikiwemo vitenganishi vitumikavyo maabara.

Rais Magufuli amesema hayo alipotembelea Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali iliyopo Kivukoni Jijini Dar es Salaam ambapo ameona jinsi mitambo ya uchunguzi vya kisasa inavyofanya kazi.

Miongoni wa uchunguzi uliokuwa ukifanywa ni pamoja na uchunguzi wa vinasaba vya miili ya watu waliopoteza maisha katika ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro  Agosti 10, 2019 baada ya lori lililobeba mafuta kupinduka na kisha kulipuka moto.

Akizungumza na wafanyakazi wa ofisi hiyo, Rais Magufuli amesema Serikali iliamua kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kununua vifaa vipya na vya kisasa, kuongeza wafanyakazi na kuibadili kutoka kuwa Wakala wa Serikali na kuwa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.

Akiwa katika maabara hiyo, Rais Magufuli amejionea mitambo mipya ya uchunguzi wa vinasaba vya binadamu, sumu, dawa za kulevya, kemikali na dawa inavyofanya kazi kwa haraka ambapo uchunguzi wa sampuli moja huchukua muda wa dakika 45 na unafanywa na vijana wa Tanzania.

“Nafahamu kuna wakati mlikuwa mnachunguza jambo na mnaandika ripoti ya uchunguzi wenu lakini hizo ripoti zilikuwa zinazimwa kwa sababu mlikuwa hamna nguvu, sasa mna nguvu nataka mfanye kazi” amesema Rais Magufuli.

Advertisement

Pia, amewataka wafanyakazi wa mamlaka hiyo kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa, kutopokea rushwa, kutotoa siri na ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha watumishi wa ofisi hiyo wanaofanya uchunguzi wa masuala mazito wanakuwa salama na hawaingiliwi katika majukumu yao.

Mapema katika taarifa yake, Dk Mafumiko amemshukuru Rais Magufuli kwa Serikali ya awamu ya tano kutoa Sh5.3 bilioni kwa ajili ya kununulia mitambo na kuongeza wafanyakazi kutoka 110 hadi 294 hali iliyoongeza ufanisi.

Mafanikio hayo kwa kipindi cha miaka minne tangu 2015 ni pamoja na vielelezo 204,974 kuchunguzwa sawa na wastani wa vielelezo 51,244 kwa mwaka, kiwango ambacho ni ongezeko la asilimia 510 ikilinganishwa na rekodi za mwaka 2015/16.

Amebainisha ufanisi wa mamlaka hiyo pia umesaidia kuongeza mahudhurio mahakamani kutoka kesi 35 kwa mwezi (2015) hadi kufikia kesi 220 kwa mwezi mwaka huu (2019) na imeongeza ofisi nyingine 2 za Kanda ya Kati na Kanda ya Kusini hali iliyorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Advertisement