Salum Mwalimu: Nimefikishwa mahakamani bila kutoa maelezo polisi

Tuesday December 3 2019

 

By Pamela Chilongola na Mainda Mhando, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu ameieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne Desemba 3, 2019 jinsi alivyofikishwa mahakamani bila maelezo yake kuchukuliwa polisi.

Mwalimu na viongozi wanane wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 112/2018 yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi katika mahakama hiyo.

Naibu katibu mkuu huyo ameeleza hayo baada ya mkurugenzi msaidizi wa mashtaka, Joseph Pande kumhoji kutokana na utetezi aliowasilisha mahakamani hapo.

Pande alimuuliza sababu za maelezo yake kufikishwa mahakamani bila kupitia polisi, Mwalimu kujibu kuwa aliletwa mahakamani na polisi lakini hakuchukuliwa maelezo yeyote.

Mkurugenzi msaidizi huyo wa mashtaka alimuuliza tena Mwalimu lini alikamatwa lakini shahidi huyo alijibu hajawahi kukamatwa na polisi.

Mwalimu alipoongozwa na wakili wa utetezi, Peter Kibatala ameieleza mahakama hiyo Februari 16, 2018 wakiwa kwenye mkutano wa kufunga kampeni za ubunge jimbo la Kinondoni, alimsikia  Mbowe akitoa maneno kumuombea kura na kumpamba.

Advertisement

"Nilimsikia Mbowe aliponinyanyua akiongea maneno ya kuniombea kura na kunipamba na si vinginevyo," amesema Mwalimu aliyekuwa akigombea ubunge kwa tiketi ya Chadema.

Mbali na Mbowe na Mwalimu, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini); John Mnyika (Kibamba); Halima Mdee (Kawe); John Heche(Tarime Vijijini); Ester Bulaya (Bunda) na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na makosa 13 likiwemo la kula njama  ambapo wote wanadaiwa kuwa  Februari Mosi na 16, 2018 Dar es Salaam walikuĺa njama ya kutenda kosa la kufanya mkusanyiko usio halali na kukiuka tamko kutawanyika.

Advertisement