Serikali Tanzania yawaondoa hofu wafanyabiashara

Sunday February 16 2020

 

By Stephano Simbeye, Mwananchi [email protected]

Mbozi. Serikali ya Tanzania imewaondoa hofu wafanyabiashara  waliokuwa wakikumbana na vikwazo wakati wa kusafirisha mizigo kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Zambia, kubainisha kuwa vitamalizika hivi karibuni.

Hayo yameelezwa leo Jumapili Februari 16, 2020 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki katika uzinduzi wa kitabu cha mwongozo wa uwekezaji kwenye kongamano la uwekezaji mjini Songwe.

Amesema vikwazo ambavyo wafanyabiashara wamekuwa wakivipata Zambia ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kupitisha mizigo kwenda DRC itamalizwa baada ya waziri wa viwanda na biashara na mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa kuanza mazungumzo na mawaziri wa  Zambia.

“Tayari mazungumzo hayo yameanza hatua ambayo inatupa matumaini ya kufikia mwafaka ambao utaondoa vikwazo vya kupitisha mizigo kwa wenzetu Zambia,” amesema Kairuki.

Waziri huyo ameziagiza  halmashauri za wilaya nchini kutenga maeneo ya uwekezaji na kuyawekea miundombinu muhimu ili kuwapunguzia kazi wawekezaji.

Mwakilishi wa kituo cha uwekezaji nchini (TIC),  Abbakari Ngwata ametoa wito kwa wakazi wa Mkoa wa Songwe licha ya kuzalisha mahindi kwa wingi kwa ajili ya chakula na biashara, waanze kulima mazao ya soko la kimkakati.

Advertisement

"Tanzania ni nchi inayounganisha masoko muhimu likiwemo lile nchi za Afrika Mashariki na soko la nchi wanachama wa Sadc lenye watu 460milioni likitumika tunaweza kupiga hatua,” amesema Ngwata.

 

Advertisement