Sh116 milioni zampeleka mkandarasi jela miaka saba

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu mkandarasi wa majengo, Alfred Ndeka (60) kifungo cha miaka saba jela baada ya kukutwa na hatia ya kujipatia Sh116 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuhukumu mkandarasi wa majengo, Alfred Ndeka (60) kifungo cha miaka saba jela baada ya kukutwa na hatia ya kujipatia Sh116 milioni kwa njia ya udanganyifu.

Hukumu hiyo imetolewa leo Jumatano Februari 19 , 2020 na Hakimu mwandamizi, Vicky Mwaikambo baada ya kuridhishwa na ushahidi wa  mashahidi watano wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo 11 vilivyowasilishwa mahakamani hapo.

Mwaikambo amesema mtuhumiwa alitenda kosa hilo na anahukumiwa kifungo cha miaka saba jela ili iwe fundisho kwa wengine.

“Kutokana na ushahidi pamoja na vielelezo vilivyotolewa unadhibitisha ulipokea Sh116 milioni kwa njia ya udanganyifu huku ukijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria hivyo mahakama hii inakuhukumu kwenda miaka saba jela,” amesema Mwaikambo.

Baada ya kumtia hatiani, wakili Mwenda aliiomba mahakama hiyo impe mshtakiwa adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama za mshtakiwa huyo.