VIDEO: Simbeye aeleza alivyomshawishi Mufuruki kuwa mwenyekiti TPSF

Mkurugenzi wa Taasisi Binafsi Nchini Tanzania (TPSF) Godfrey Simbeye akitoa salamu za rambirambi wakati wa kuagwa kwa mwili wa mfanyabiashara maarufu Ali Mufuruki jijini Dar es Salaam leo.

Muktasari:

Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi Binafsi Nchini Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye ameeleza namna alivyomshawishi bila mafanikio mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki kuwa mwenyekiti wa taasisi hiyo.

Dar es Salaam. Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi Binafsi Nchini Tanzania (TPSF), Godfrey Simbeye ameeleza namna alivyomshawishi bila mafanikio mfanyabiashara maarufu nchini, Ali Mufuruki kuwa mwenyekiti wa taasisi hiyo.

Simbeye ametoa kauli hiyo leo Jumanne Desemba 10, 2019 katika shughuli ya kuaga mwili wa Mufuruki aliyefariki dunia juzi nchini Afrika Kusini iliyofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Huku akitokwa machozi, Simbeye amesema Mufuruki amefariki dunia kabla hajafanikiwa kumshawishi kuwa mwenyekiti wa taasisi hiyo.

"Mufuruki amekuwa kwenye bodi nyingi lakini kuna kitu hajakifanya na nilitamani akifanye lakini hakijatokea," amesema Simbeye.

Amesema TPSF ilitamani mfanyabiashara huyo awe mwenyekiti wake, kwamba licha ya  kumfuata na kumueleza  mara kwa mara alijibu kuwa haikuwa muda wake.

"Nilimuuliza kuwa anatamani kuwa mwenyekiti wa TPSF akasema ndio ila kwa sasa ngoja kwanza Mzee Reginald Mengi (marehemu) aendelee," amesema.

Simbeye amesema juhudi zake hazikuishia hapo na hakukata tamaa, “aliniambia kuwa sio muda huu kwa sasa anahitaji kufanya mambo mengi, tulikuwa tunahitaji taasisi hii iwe na kiongozi bora atakayetoa mchango katika sekta binafsi.”