Simulizi ya Mtanzania aliyezaliwa siku ya Uhuru

Monday December 9 2019

Florencia Maurus Njalika akiwa nyumbani kwake

Florencia Maurus Njalika akiwa nyumbani kwake jijini Dar es Salaam. Alizaliwa siku ya Uhuru Desemba 9, 1961. Picha na Mpigapicha Wetu  

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

“Nimezaliwa kukiwa na amani hivyo tuiendeleze na pia tuwe na mshikamano bora katika Taifa letu lililobarikiwa na Mwenyezi Mungu,” ndivyo anavyosema Florencia Maurus Njalika ambaye leo anatimiza umri wa miaka 58.

Florencia aliyezaliwa siku ambayo Tanganyika ilipata uhuru, anasherehekea siku hii akiwa bibi mwenye wajukuu wanane kutoka kwa watoto wake wanne wote wa kike aliojaaliwa kuwazaa na mumewe Thomas Ulaya, ambaye sasa ni marehemu.

Anaadhimisha kufikisha umri wa miaka 58 huku akimshukuru Mungu kwa kumuwezesha kuwalea watoto wake wanne tangu wakiwa wadogo baada ya mumewe kufariki dunia na watoto wake hao wote sasa wameolewa.

Florencia anaifurahia siku ya leo na kumshukuru Mungu kumuwezesha kuwaona na kuwalea wajukuu wanane ambao ni matunda ya malezi mema kwa mabinti zake wanne.

Anasimulia kuwa alizaliwa Desemba 9, 1961 kwenye familia ya watoto sita ya baba Maurus Njalika na mama Leah Daudi Samkongwa.

Florencia anasema alizaliwa katika hospitali ya Mission Uwemba katika Kijiji cha Uwemba Mkoa wa Iringa (sasa Mkoa wa Njombe). Anasema kipindi cha uhuru kulikuwa na amani chini ya Rais wa kwanza, Mwalimu Julius Nyerere.

Advertisement

Anasimulia kuwa alisoma Shule ya Msingi Uwemba Mission kuanzia darasa la kwanza hadi la tano, kisha akahamishiwa Shule ya Msingi Chipole iliyokuwa chini ya masista wilayani Songea, Ruvuma kuanzia darasa la tano hadi la saba.

Florencia anasema alimaliza darasa la saba mwaka 1978, hakufaulu, lakini alijiunga na Shule ya Sekondari Highland mkoani Iringa mwaka 1979 na kumaliza kidato cha nne na kuchaguliwa katika Chuo cha Ualimu Korogwe, Tanga.

Anasema wakati huo mjomba wake John Kaziulaya Mkongwa (sasa ni marehemu) alimtafutia kazi katika Benki ya Taifa ya Biashara jijini Dar es Salaam alikotumikia kwa takriban miaka 18, hadi alipopunguzwa kazi baada ya kuingia teknolojia ya kompyuta.

Florencia anasema anamshukuru Mungu kwani baada ya kupunguzwa kazi aliamua kujihusisha na ufugaji wa kuku, biashara ambayo bado anaendelea kuifanya.

Anasema yeye ni mwanachama wa CCM na anakipenda chama chake kwa sababu ndio chama pekee chenye kuleta maendeleo na kinachojali masilahi ya wanyonge.

Florencia anasema amezaliwa ndani ya siasa za chama tawala na kwamba baba yake alikuwa diwani wa CCM na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec). Anasema pia mama yake, Leah Mkongwa aliwahi kuwa mbunge wa kuteuliwa kutoka Jimbo la Njombe, lakini kabla ya kuapishwa alifariki dunia 2008.

Florencia anasema miaka 58 ya Uhuru katika awamu hii ya tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kupitia CCM, Watanzania wana mambo mengi ya kujivunia katika sekta zote ikiwemo afya, miundombinu na elimu kwa kuwa mambo mengi yamekuwa mazuri yakiwamo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Anasema kupitia Rais Magufuli maisha yamekuwa mazuri kijamii kwa kuwa kuna huduma nzuri za hospitali, huduma nzuri za bima ya afya na pia ulanguzi wa dawa kwa sasa haupo.

Florencia anasema sasa wagonjwa wanatibiwa vizuri, rushwa iliyokuwa ikilalamikiwa kwenye hospitali nyingi imepungua na huduma za afya zimeboreshwa na hospitalini kuna vitanda na dawa.

Anasema kwenye eneo la miundombinu, barabara zimejengwa pia kuna barabara za juu, ndege mpya zimenunuliwa kwa fedha za Watanzania wenyewe, wakati huko nyuma haya hayakuonekana.

“Mimi nakaa Kiwalani kipindi cha nyuma wajawazito hadi wafike hospitali ilikuwa kazi na wengine walijifungulia njiani kutokana na ubovu wa barabara, lakini sasa barabara imejengwa kwa kiwango cha lami na inafika hadi mlangoni kwangu, hakuna mafuriko tena mitaro imejengwa,” anasema Florencia.

Anasema Rais Magufuli amewezesha uchumi kukua na sera yake ya Tanzania ya viwanda inatekelezeka kwa kuwa amezindua miradi mingi mikubwa kama ujenzi wa bwawa la umeme la Rufiji (Stiegler’s Gorge), mradi wa reli ya umeme (Standard Gauge Railway) na viwanda vimeanzishwa vingi vidogo na vikubwa.

Florencia anasema maisha yamekuwa sawa kwa kuwa pengo la matajiri na maskini limepungua, na hiyo inatokana na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.

Pia, anasema kupitia utawala wa sasa kodi zinakusanywa ipasavyo na kuna usimamizi mzuri wa fedha za umma na yote ni kwa sababu Tanzania ina Rais mchapakazi.

“Katika miaka hii 58 ya uhuru pamoja na siku nzuri ya baraka ya kuzaliwa kwangu nawaomba Watanzania wenzangu tuziunge mkono juhudi zote za maendeleo anazozifanya Rais wetu mpendwa John Magufuli mpenda wanyonge, anayefanya kazi bila kuchoka katika kutatua kero za Watanzania bila kubagua dini wala kabila. Kwa upande wangu naiona kesho ya Tanzania ikiwa yenye mafanikio tumuombee sana.

“Kwa yote anayofanya sisi pia tumuunge mkono kwa kufanya kazi na tuidumishe kaulimbiu yake ‘hapa kazi tu’. Hivyo, tufanye kazi kwa bidii kwa msingi wa Taifa letu hata Mungu anasema asiyefanya kazi na asile pia tudumishe amani yetu.

“Katika uzalendo naiona kesho yenye mafanikio na uchumi mkubwa kwa Taifa letu,” anasema Florencia ambaye leo anasherehekea siku yake ya kuzaliwa.

Advertisement