Taasisi za elimu zishirikiane na sekta ya ajira kuleta tija ya elimu

Tangu mwaka 1948, elimu imetambulika na Umoja wa Mataifa kama miongoni mwa haki za msingi za binadamu. Elimu inapaswa kukuza utu, ustawi wa binadamu, kujenga msingi wa watu kutambua uhuru wao, haki na usawa kwenye jamii na kupambana na maadui wanaohatarisha ustawi wao kiuchumi, kisiasa, na kimaendeleo.

Elimu inayotolewa inapaswa kukuza tija katika uzalishaji, rasilimali watu, kipato, ajira na maendeleo ya kiuchumi ya mtu binafsi na taifa kwa ujumla.

Faida binafsi kwa mtu aliyesoma ni pamoja na nafasi ya kuajirika, kuongezeka kwa ubora katika uzalishaji, ongezeko la kipato na kupungua kwa umaskini.

Faida nyingine ya elimu kwa jamii ni pamoja na kuongezeka kwa tija katika uzalishaji na biashara, kuwa na maendeleo ya muda mrefu pamoja na ubunifu unaolenga kuondoa kero na matatizo yanayoikabili jamii husika.

Hata hivyo kwa miaka mingi sasa wadau wengi wamekuwa wakieleza wasiwasi wao kuwa elimu inayotolewa kwa vijana wa kitanzania bado haijakidhi mahitaji ya jamii na sekta ya ajira na ile ya uzalishaji.

Hali ilivyo kwenye mfumo wetu wa elimu

Wadau mbalimbali na mashirika mbalimbali ya kimataifa na ya ndani ya nchi kama vile UNESCO, Benki ya Dunia, HakiElimu, Twaweza pamoja na taasisi za sekta binafsi kwa nyakati tofauti wamekuwa wakieleza kuwa elimu inayotolewa Tanzania bado haijakidhi mahitaji ya soko la ajira na wahitimu wengi wamekosa sifa za kuajirika.

Sababu zinazoelewa na wadau wengi kuwa zimechangia kushuka kwa kiwango cha ubora wa elimu nchini ni pamoja na ufinyu wa bajeti, mazingira ya kufundishia na kujifunza kutokuwa rafiki.

Pia kuna usokefu wa ushirikiano kati ya taasisi za elimu na sekta ya ajira kwa ajili ya kuandaa pamoja mitalaa itakayowasadia vijana kusoma huku wakiendana na mahitaji ya soko la ajira.

Kwa nini sekta ya elimu na sekta ya ajira lazima zishirikiane?

Taasisi za elimu nchini ni kama mpishi anayepika chakula na walaji wa hicho chakula ni sekta ya ajira.

Mpishi asipojua mahitaji ya walaji wake basi anaweza akapika chakula kisichovutia wateja wake.

Lakini pia kwa upande wa pili, ikitokea mlaji haelezi anachotamani kupikiwa basi mpishi hataweza kubadilika na atabaki na aina moja ya upishi maisha yote ya kazi.

Kwa muda mrefu sasa, sekta binafsi imekuwa ikipaaza sauti kuwa vyuo vikuu na vyuo vya kati nchini haviwaandai wahitimu wazuri au wahitimu wenyewe hawajiandai vizuri kwa soko la ajira.

Hata hivyo haitoshi kuvilaumu vyuo pekee kwa suala hilo kwani miaka ya mwanafunzi kuwepo chuo haitoshi kumpa mhitimu kila aina ya ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira.

Si hivyo tu, bali pia vyuoni wanafunzi kwa sehemu kubwa wanafundishwa mambo mengi kwa nadharia zaidi.

Wamekuwa na muda kidogo sana wa kufanya mazoezi kwa vitendo. Na kwa bahati mbaya pia mfumo wa mazoezi kwa vitendo haujaonyesha kuwa na tija kubwa kwao kwasababu kutokana na ufinyu wa bajeti wanakaa kwenye vituo vya mafunzo kwa muda mfupi na pia wanakosa walimu wa kuwasimamia kwa ukaribu katika mafunzo hayo.

Ipo haja sasa kwa sekta ya ajira na sekta ya elimu kukaa pamoja kubainisha mahitaji ya mafunzo vyuoni na kushirikiana bega kwa bega na taasisi za elimu katika kuandaa programu za pamoja za mafunzo.

Lengo la kuwa na programu za ushirikiano huo ni kuhakikisha kuwa mafunzo ya nadharia yaende sambamba na mafunzo kwa vitendo.

Faida ya kuwa na programu hiyo ni kuwa sekta ya ajira itapata nguvu kazi kutoka kwa wanafunzi wa vyuoni na wakati huo huo kuwaandaa kama waajiriwa wa baadaye na hivyo kupunguza gharama za mafunzo kazini kwakuwa watakuwa tayari wamepata uzoefu wakati wa kuendesha mafunzo kwa vitendo.

Namna ya kuendesha programu za ushirikiano

Tunaweza kujiuliza tunafanyaje kipya wakati tayari tuna mfumo wa mafunzo ya vitendo wakati wa likizo ambapo wanafunzi wanaenda kwenye taasisi au makampuni mbalimbali kujifunza?

Ni kweli huo mfumo wa mafunzo kwa vitendo si mbaya lakini napendekeza maboresho zaidi katika kuendesha programu za ushirikiano kati ya sekta ya elimu na sekta ya ajira. Ninapendekeza namna mbili za kufanya.

Njia ya kwanza ni ile ambayo inafanana na namna vyuo vya udaktari wanafanya.

Chuo kikuu kinabainisha programu zilizopo katika chuo chake na sekta zinazohusiana na programu hizo.

Wakishabainisha sekta hizo wanakaa meza moja na wadau wote na kubainisha mahitaji ya maarifa yanayohitajika kwa kila sekta.

Baadaye chuo husika kinafanya mapitio ya programu zake na kuongeza masomo ambayo sekta ya ajira inataka.

Chuo kikishafanya hivyo, kinaandaa mfumo wake wa ufundishaji ambao utaruhusu wanafunzi kwenda kwenye sekta husika kufanya kazi muhula mzima au kipindi fulani kirefu ambacho watakubaliana na wadau wa kwenye sekta husika.

Hapa namaanisha kwa mfano mwanafunzi wa uhandisi wa mitambo, atasoma semesta moja darasani mada kadhaa ambazo zitamwandaa kwenda kufanyia mazoezi kiwanda fulani. Au kama ni mwanafunzi wa uandishi wa habari basi anasoma mada kadhaa na baadaye anaenda kutumia maarifa hayo kivitendo kwenye chombo fulani cha habari kwa muhula unaofuata. Halafu anarudi chuo kufanya mitihani ya kumaliza mwaka. Mtihani uwe na kipengele cha nadharia na kipengele cha vitendo.

Akishamaliza mwaka mmoja kwa mfumo huo anaingia mwaka wa pili kwa kufundishwa mada nyingine tofauti ambazo nazo zitamwandaa kwenda kwenye sekta ambayo itaweza kumwajiri. Muhula wa pili anautumia kwenye mazoezi kazini ambako mbali na kupata nafasi ya kutumia maarifa aliyopata darasani bali pia atajifunza stadi tepe (soft skills) ambazo hakuweza kujifunza chuoni.

Kwa njia hii tutawaandaa vizuri wahitimu wetu ambao watakuwa na maarifa yaliyowiana na hata pia kujenga mtandao wa ajira na kujiajiri.

Pia utakuwa mfumo wenye faida kwa waajiri kwasababu watakuwa na fursa ya kuwachunguza hao wanafunzi na kuona mapema wenye sifa za kuajirika na pia kupunguza gharama za kutoa mafunzo. Pia tusisahau kuwa watakuwa wanatoa mchango wa nguvu kazi.

Ili kufanikisha hilo, tunahitaji serikali na vyuo kutenga rasilimali za kutosha. Mbali na hilo, pia vyuo vitatakiwa pia kuangalia athari za muda wa wanafunzi kukaa vyuoni.

Tunaweza kufikiria kuongeza mwaka au miezi kadhaa katika mfumo wa sasa wa mafunzo vyuoni.

Namna ya pili ya kufanya ambayo inaweza isiwe na gharama kubwa ni ile ya kutoa nafasi ya wanafunzi kila wiki kufanya kazi za kujitolea kwenye sekta husika na wanachosomea. Hapa namaanisha kuwa vyuo baada ya kukutana na wadau wa sekta ya ajira na kubainisha mahitaji yao ya maarifa, basi vyuo vitatakiwa kutenga siku mbili au tatu ambazo zitakuwa huru kwa wanafunzi kuwa nje ya masomo na kwenda kujitolea kwenye sekta husika.

Faraja Kristomus ni mhadhiri Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. 0787525396