Takukuru yamnasa Mhandisi wa Halmashauri ya Nyasa kwa rushwa

Tuesday June 25 2019

 

By Joyce Joliga, Mwananchi [email protected]

Songea. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa  (Takukuru) mkoa wa Ruvuma, inamshikilia mhandisi wa maji wa halmashauri ya wilaya ya Nyasa mkoani humo, Evaristo Ngole kwa kosa la kushawishi  na kupokea rushwa ya Sh9 milioni kutoka kwa mkandarasi.

Akizungumza na Mwananchi jana Jumatatu Juni 24, 2019,  Mkuu wa Takukuru mkoa wa Ruvuma, Yustina Chagaka alisema mhandisi huyo aliomba fedha hizo kutoka kwa mkandarasi ili aweze kumpitishia  malipo yake ya kazi ambazo alizokuwa amefanya katika wilaya hiyo.

Alisema mkandarasi huyo alitekeleza mradi wa maji katika vijiji vya Lilondo, Asili pamoja na Lumecha na  kukamilika kwa wakati  kutokana na mkataba wake wa kazi, alidai wakati akisubiri kulipwa malipo yake ndipo mhandisi huyo alipofikia hatua ya kumshawishi kwa kumwomba kiasi hicho cha fedha na kumtaka akaziingize katika akaunti yake iliyopo benki ya CRDB.

   Alisema mlalamikaji ambaye ndiye mkandarasi wa mradi huo wa maji katika vijiji hicho vitatu vya wilaya hiyo ya Nyasa alidai aliingiza fedha hizo kwenye akaunti hiyo kwa awamu  tatu, ndipo alipoweza kuwekewa mtego na kufanikiwa kukamatwa baada ya fedha hiyo kuingia kwenye akaunti yake.

 Chagaka alisema baada ya fedha hizo kuingia kwenye akaunti yake na kufanya uchunguzi waliweza kubaini ukweli.

Alidai tayari amekamatwa na anahojiwa na maofisa wa taasisi hiyo kwa kosa la kushawishi na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana  na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.

Advertisement

Alisema Takukuru mkoa wa Ruvuma inatoa pongezi kwa wakandarasi wote ambao wanazingatia weledi katika kutekeleza miradi ya maendeleo ili thamani ya fedha iweze kuonekana katika miradi hiyo kuleta tija kwa Taifa.

Advertisement