Tanzania yapata mkopo wa Sh3 trilioni ujenzi reli ya kisasa

Thursday February 13 2020

 

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesaini mkopo wa Sh3.3 trilioni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa reli la kisasa (SGR) awamu ya pili kutoka Morogoro, Makutupora na Singida.

Mkopo kwa ajili ya mradi huo umeratibiwa na benki ya Standard Chartered na umejumuisha wakopeshaji 17 ikiwemo Serikali ya Denmark na Sweden.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini leo Alhamisi Februari 13, 2020, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema Serikali itasimamia fedha hizo kuhakikisha zinatumika kama ilivyopangwa.

“Mkopo huu tutaurejesha ndani ya miaka 20 kwa hiyo muda tunao, nawashukuru wabia hawa ambao wameunga mkono jitihada za Serikali za kubadilisha uchumi wa nchi kwa kutupatia mkopo huuwa Sh3.3 trilioni, tunawashukuru sana na mtabaki katika mioyo ya Watanzania.”

“Wale wanaosema deni la Taifa  linakuwa waambie tu kuwa deni ni himilivu, tunachukua mkopo na tutaulipa.  Kuna baadhi ya wabia tuliwaomba watuchangie mkopo kwa ajili ya mradi huu walikataa, hivyo tunaishukuru sana benki hii kwa kuratibu zoezi hili,” amesema.

Mkurugenzi mtendaji wa benki ya Standard Chartered, Sanjay Rughani amesema mkopo umetolewa kuunga mkono sera ya viwanda.

Advertisement

“Tutaendelea kushirikiana na Serikali katika miradi mbalimbali ya maendeleo miradi mbalimbali, kwani nimeona nikiendeleza uchumi wa nchi hata biashara yangu itakuwa,” amesema.

 

Advertisement