Upande wa utetezi kutumia video kumhoji shahidi kesi ya kina Mbowe

Tuesday August 20 2019

Katibu Mkuu , Chadema, Dk Vicent Mashinji,Koplo Charles,mwenyekiti,Mahakama  ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam ,Freeman Mbowe,

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe  

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeridhia ombi la upande wa utetezi kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema, akiwemo mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Freeman Mbowe kutumia ushahidi wa video kumhoji shahidi.

Mbowe na viongozi wengine wanane wa chama hicho wakiwemo wabunge sita, wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 112/2018 yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi.

Wakili wa utetezi Peter Kibatala ametoa ombi hilo leo Jumanne Agosti 20, 2019  mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya upande wa utetezi kumhoji shahidi wa sita wa upande wa mashtaka ambaye ni askari polisi mwenye namba F 5392 Koplo Charles.

Video hiyo ilitolewa jana Jumatatu Agosti 19, 2019 mahakamani hapo na Charles, wakati akitoa ushahidi wake dhidi ya washtakiwa hao.

“Kwa kuwa shahidi wa upande wa mashtaka baadhi ya maswali tunayomuuliza anasema hakumbuki labda mpaka turudie  kuangalia mkanda wa video ulioonyeshwa jana mahakamani hapa.”

“Tumeona ni vyema mahakama yako ikaturuhusu na kutupa mazingira wezeshi ya kwenda kuangalia tena video ile ili na sisi tuweze kumuuliza maswali yetu vizuri shahidi huyu,” amesema Kibatala.

Advertisement

Hakimu Simba baada ya kusikiliza ombi hilo, alikubaliana na upande wa utetezi wa kuruhusu video hiyo ionyeshwe tena katika ukumbi wa mikutano  na mafunzo uliopo katika Mahakama ya Kisutu.

Hakimu Simba baada ya kueleza hayo, ameahirisha kesi hiyo kwa muda wa dakika 35 kupisha maandalizi ya kufunga projekta.

Awali, kesi hiyo kuahirishwa kwa muda na wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi alieleza mahakama hiyo kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya upande wa utetezi kumhoji mshtakiwa.

Nchimbi baada ya kueleza hayo, Kibatala alianza kumhoji shahidi huyo kama ndio mara yake ya kwanza kutoa ushahidi, ambapo Koplo Charles alidai sio mara yake ya kwanza kutoa ushahidi.

Pia alihojiwa sababu ya yeye kuondoka katika mkutano wa Chadema ambao ulikuwa ni wa kufunga pampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni.

Shahidi huyo amedai aliondoka baada ya kuona wananchi na viongozi wa Chadema wanaondoka kuelekea  katika ofisi za mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni kudai barua za viapo vya mawakala wa kusimamia uchaguzi wa chama hicho.

Mbali na Mbowe washitakiwa wengine ni Katibu Mkuu Chadema Dk Vicent Mashinji;  naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi

 


Advertisement