Ushahidi wa video kuonyeshwa mahakamani kesi ya kina Mbowe

Monday August 19 2019

mwenyekiti wake, Freeman Mbowe,Ushahidi wa video kuonyeshwa mahakamani kesi ya kina Mbowe

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeamuru kuonyeshwa kwa video iliyopokelewa mahakamani hapo kama ushahidi katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema akiwemo mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu, Agosti 19, 2019 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, baada ya kupitia hoja za upande zote mbili.

Uamuzi huo unatokana na upande wa utetezi kupinga video hiyo isionyeshwe mahakamani hapo kutokana na upande wa mashtaka kushindwa kuandaa mazingira wezeshi.

Video hiyo iliyochukuliwa katika ufungaji wa kampeni za uchaguzi mdogo  wa ubunge wa Kinondoni kwa tiketi ya Chadema Februari 16 mwaka 2018.

Akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba amesema sababu zilizotolewa na upande wa utetezi haina mashiko, hivyo video hiyo inatakiwa ionyeshwe katika ukumbi wa Tehama uliopo katika mahakama ya Kisutu.

"Hivyo kwa sababu hiyo, Mahakama inaamuru kuwa video hiyo ionyeshwe kupitia vifaa maalum vilivyopo katika ukumbi wa mikutano wa Tehama uliopo mahakamani" amesema Hakimu Simba na kuahirisha kesi hiyo kwa muda wa dakika 20 kwa ajili ya maandalizi ya kuangalia video.

Advertisement

Awali, wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amedai kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya Mahakama kutoa uamuzi na wako tayari kusikiliza uamuzi huo.

Itakumbukwa, Julai 26, 2019, upande wa utetezi ulipinga kuonyesha kwa mkanda wa video uliotolewa na upande wa mashtaka mahakama.

Wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala alidai upande wa mashitaka ulipaswa kuandika barua kwa uongozi wa mahakama kuomba kutumika kwa kituo cha mafunzo kuonesha maudhui  yaliyopo katika mkanda huo wa video.

Kibatala alidai, upande wa mashtaka walipaswa kuandaa vifaa vyote muhimu ikiwemo waya na projekta ambavyo vingewezesha kuonekana kwa video hiyo na sio wajibu wa mahakama kuandaa.

Mbali na Mbowe washitakiwa wengine ni Katibu Mkuu Chadema, Dk Vicent Mashinji, Naibu Katibu Wakuu, John Mnyika (Bara) na Salumu Mwalimu (Zanzibar).

Wengine ni wabunge, Ester Matiko (Tarime Mjini), Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda Mjini), John Heche (Tarime Vijijini) na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, yakiwemo ya uchochezi, wanayodaiwa kutenda Februari 16, 2018, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni.

Endelea  kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi


Advertisement