Utamu EPL

Muktasari:

Baada ya kipute hicho cha mchana, mashabiki wa mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England, hii leo Jumamosi watashuhudia shughuli nyingine pevu huko Etihad wakati Pep Guardiola na chama lake la Manchester City atakapokuwa nyumbani kuikaribia Arsenal, inayonolewa na aliyekuwa msaidizi wake, Mikel Arteta.

LONDON, ENGLAND. UTAMU wa Ligi Kuu England unarudi tena, huku macho ya wengi yakiwa Goodison Park na Etihad.

Huko Goodison Park kinakwenda kupigwa kipute cha Merseyside Derby, wakati Everton kwenye ubora wake chini ya Carlo Ancelotti itakapowakaribisha mabingwa Liverpool chini ya Mjerumani wao Jurgen Klopp. Vuta nikuvute. Utamu wa ligi unarudi baada ya mapumziko ya mechi za kimataifa.

Baada ya kipute hicho cha mchana, mashabiki wa mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England, hii leo Jumamosi watashuhudia shughuli nyingine pevu huko Etihad wakati Pep Guardiola na chama lake la Manchester City atakapokuwa nyumbani kuikaribia Arsenal, inayonolewa na aliyekuwa msaidizi wake, Mikel Arteta. Mechi hiyo inaaminika kuwa na mvuto mkubwa kutokana na uhusiano wa makocha wao, lakini kwa mechi zilizopita, Man City imekuwa mbabe kwa Arsenal. Man City imeshinda mechi sita za mwisho za ligi ilizocheza dhidi ya Arsenal, tena kwa tofauti na mabao mawili na zaidi, ikiwamo ushindi wa 3-0 kwenye mechi zote mbili za nyumbani na ugenini msimu uliopita. Hata hivyo, Arsenal haijawahi kupoteza mechi saba mfululizo kwenye ligi dhidi ya timu moja tangu 1977, hivyo wababe hao wa London wanaweza kupindua mechi.

Kuhusu kipute cha Merseyside, Everton itasaka ushindi wake wa kwanza baada ya miaka 10, huku msimu huu ikionekana kuwa kwenye kiwango bora kabisa chini ya kocha Ancelotti na mastaa James Rodriguez na straika, Dominic Calvert-Lewin - anayefunga kama anavyojisikia. Kwenye ligi msimu huu, Everton imeshinda mechi zote nne, huku ikifunga mabao 12 na kufungwa matano, wakati Liverpool imechapwa mara moja, imefunga mabao 11 na kufungwa 11.

Shughuli nyingine ya mikikimikiki hiyo ya Ligi Kuu England kwa siku ya leo itakuwa huko St James’ Park, wakati Manchester United itakapokuwa ugenini kuona kama itaweza kurudi kwenye ubora wake mbele ya Newcastle United baada ya kuchapwa 6-1 na Tottenham kwenye mchezo uliopita. Man United imecheza mechi tatu kwenye ligi hiyo, ikichapwa mara mbili na kushinda moja tu kwa mbinde, huku kikosi hicho kikiruhusu wavu wao kuguswa mara 11 na wao wakifunga mabao matano pekee, kitakuwa ugenini kwa Newcastle United, ambapo kwenye mechi nne walizocheza, wameshinda mbili, sare moja na kupoteza moja, wakifunga mabao sita na kufungwa matano. Mechi hiyo inatajwa kuwa ni moja kati ya nyingi zitakazopigwa ndani ya wiki tatu ambazo zinaelezwa kushikiria kibarua cha kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Frank Lampard na chama lake la Chelsea atakuwa nyumbani Stamford Bridge kukipiga na Southampton, ikiwa ni kipute cha London derby, huku kesho Jumapili, kutakuwa na mechi nne matata kabisa, Sheffield United wakiwa nyumbani kucheza na Fulham, Crystal Palace wakiwakaribisha Brighton, Leicester City wakijitupa King Power kuwakaribisha watemi wa Liverpool, Aston Villa wakati Jose Mourinho na chama lake la Spurs atakuwa nyumbani kucheza na West Ham United katika kipute kingine cha London derby.

Jumatatu kutakuwa na mechi mbili tu, West Brom wakikipiga na Burnley huku kocha Marcelo Bielsa ya Leeds United yake akiwa na shughuli nzito kwa Wolves. Kwenye mechi hizo za Ligi Kuu England wikiendi hii, kuna wachezaji watano wanaweza kucheza mechi zao za kwanza, Thomas Partey akitarajia kuichezea Arsenal kwa mara ya kwanza, huku Alex Telles akitarajia kuonekana kwenye kikosi cha Man United. Rhian Brewster anatarajia kuonekana kwenye jezi ya Sheffield United, Ruben Loftus-Cheek kwenye uzi wa Fulham na Gareth Bale, akitarajia kuichezea Spurs kwa mara ya kwanza baada ya kurudi kuitumikia timu hiyo akitokea kwa mkopo Real Madrid.