Advertisement

Utaratibu wa kuapishwa mawakala walalamikiwa, NEC yaongeza muda

Wednesday October 21 2020
makaaalapic

Mawakala wa vyama mbalimbali kutoka majimbo ya Kinondoni na Kawe

Dar es Salaam. Wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani wamelalamikia utaratibu unaotumika kuapisha mawakala na kuomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuongeza muda.

Kwa mujibu wa utaratibu uliotolewa na NEC, vyama vya siasa vinatakiwa kuandaa mawakala wakiwa na picha au nakala ya kitambulisho cha kupiga kura, leseni ya udereva au kitambulisho cha Taifa watakaoapishwa siku saba kabla ya tarehe ya uchaguzi.

Hata hivyo NEC imeongeza muda wa mawakala kuapishwa kwa siku mbili hadi Oktoba 23, 2020

VIDEO: NEC yaongeza siku mbili za kuapisha mawakala

Mwananchi imepita katika vituo mbalimbali na kushuhudia umati wa mawakala wakisuburi kuapishwa huku wagombea wakilalamikia utaratibu wa kukusanya mawakala wa vyamaa vyote kwenye kituo kimoja.

Mgombea udiwani wa Hananasifu kwa tiketi ya Chadema Ray Kimbita ameiomba NEC kutoa muda wa ziada ili mawakala ambao hawajaapishwa waapishwe.

Advertisement

Amesema utaratibu uliokuwa unaotumika miaka ya nyuma mawakala walijua wanaapishwa kwenye ofisi za watendaji wa kata tofauti na utaratibu wa mwaka huu.

"Kuna vyama kumi na sita vinavyoshiriki uchaguzi kitendo cha kurundika mawakala sehemu moja kinasababisha mawakala wengine washindwe kuapishwa kutokana na kazi,"amesema Kimbita.

"Taarifa tumeipata jana, sisi tumezoea ule utaratibu wa zamani kawaida taarifa zinakuwepo tangu mwanzo na hakuna mazingira yoyote yaliyoandaliwa.”

Kimbita amesema hakuna sababu ya watendaji wa kata kutoka kwenye ofisi zao na kwenda kuwaapishia sehemu moja kitendo hicho ni maandalizi mabovu ya tume.

"Tume ilitakiwa kuandaa mazingira ya watu wamekalishwa kwenye jua na hatujui tutakaa hadi sanga, tunaomba zoezi hili liendelee kwa siku nne kuanzia asubuhi hadi saa 12 jioni au warudishe utaratibu wa zamani mawakala kuapa kwenye kata zao,"amesema.

Mgombea ubunge wa Kawe kwa tiketi ya NLD,  Emmanuel Mwankina amesema utaratibu wa mwaka huu umekuwa tofauti kutokana na utaratibu uliotumika wa kukusanya mawakala sehemu moja kutoka kwenye kata mbalimbali.

Amesema zoezi hilo linachangia kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwamo ya kukusanya watu wengi kwenye eneo moja na kusababisha kuchukua muda mrefu na wengine kukata tamaa na kuondoka.

"Baadhi ya mawakala walikuja ili waape na kisha kuendelea na shughuli zao, hata baadhi ya mawakala wangu wameniomba kuondoka zoezi hili lina changamoto kubwa sana tume itengeneze utaratibu mzuri,"amesema Mwankina.

Mwankina ameiomba tume kuongeza muda na kutengeneza mazingira rafiki ili mtu akifika aapishwe na kuondoka badala ya kuweka watu kwa saa nyingi kusubiri kuapishwa.

Msimamizi msaidizi wa Kawe, Halima Kahema amesema jumla ya vyama vinavyoshiriki kuapisha mawakala ni 17 na msimamizi wa uchaguzi ni mmoja.

Utaratibu wa kukusanya mawakala wote katika kituo kimoja ni kugawa kazi kwa wasimamizi wasaidizi ili kazi ya uwapishaji ifanyike kwa urahisi.

Advertisement