Breaking News

Utatu huu Simba balaa

Friday October 16 2020

 

By CHARLES ABEL

MASHABIKI wa Simba walikuwa na mzuka mwingi baada ya Bernard Morrison kuwapiga chenga ya mwili watani wao, Yanga kwa kuwakacha Jangwani na kutua Msimbazi, lakini ghafla mambo yamekuwa sivyo kwa winga huyo, ila imebainika kilichomponza Mghana huyo.

Kama hujui ndani ya Simba kwa sasa kuna utatu wa kibabe unaoundwa na nyota watatu wa kigeni, Clatous Chama, Larry Bwalya na Lui Miquissone uliofanya baadhi ya nyota waliotamba msimu uliopita ndani ya kikosi cha kwanza kupotezwa sambamba na BM3 aliyetabiriwa makubwa ndani ya timu hiyo.

Utatu huo katika safu ya kiungo ya Simba ndio unaoongoza kwa kuzalisha idadi kubwa ya mabao katika Ligi Kuu, pia takwimu zao kwa upande mwingine zinawaweka katika wakati mgumu nyota watano wa timu hiyo, akiwamo Morrison ambaye mashabiki walimtabiria angetamba baada ya kutua Msimbazi.

Simba imekuwa ikipendelea kutumia zaidi mfumo wa 4-2-3-1 ambao unakuwa na viungo wawili wa ulinzi na juu yao wanakuwepo viungo watatu wa ushambuliaji wanaocheza nyuma ya mshambuliaji wa kati.

Katika mfumo huo wa kuwatumia viungo watatu wa ushambuliaji, kocha Sven Vandenbroeck awali msimu huu alikuwa akiwatumia Morrison, Chama na Hassan Dilunga katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo, pia katika mechi mbili za mwanzo za Ligi Kuu dhidi ya Ihefu na Mtibwa Sugar.

Kwenye mechi hizo, Miquissone hakupangwa kutokana na kuchelewa kujiunga na timu hiyo baada ya kwenda kwao Msumbiji kuoa, huku Bwalya akiwekwa benchi kwa kile kilichoonekana kutozoea mazingira ya viwanja vilivyotumika kwa mechi hizo.

Advertisement

Utatu huo wa Dilunga, Chama na Morrison ulihusika na mabao matatu tu katika mechi hizo tatu ambazo Simba ilifunga mabao matano ambayo yalikuwa ni katika mchezo dhidi ya Namungo FC walioibuka na ushindi wa mabao 2-0 (la kwanza likitokana na penalti baada ya Morrison kuangushwa ambayo ilifungwa na John Bocco na baadaye nyota huyo kutoka Ghana akapachika la ushindi na ule dhidi ya Ihefu ambao Chama alipika bao la Mzamiru Yassin katika ushindi wa mabao 2-1 walioupata).

Hata hivyo, baada ya utatu uliowajumuisha Dilunga, Morrison na Chama kuonekana hauna ufanisi mkubwa, benchi la ufundi la Simba liliamua kubadili kikosi na kuwarudisha benchi Dilunga na Morrison huku likiwaingiza Miquissone na Bwalya katika kikosi cha kwanza.

Uwepo wa watatu hao katika kikosi cha kwanza cha Simba katika mechi tatu dhidi ya Biashara United, Gwambina na JKT Tanzania ambao timu hiyo ilitumia mfumo wa 4-4-2 umeonekana kuwa hatari zaidi huku ukizidi kuondoa uwezekano wa Morrison na Dilunga walioanza vizuri, kurejea kikosi cha kwanza.

Katika mechi hizo tatu, ambazo Simba imeshinda zote na kupachika jumla ya mabao 11, Bwalya, Luis na Chama kwa pamoja wamezalisha jumla ya mabao 10 huku moja tu wakiwa hawajahusika nalo.

Mechi dhidi ya Biashara ambayo Simba waliibuka na ushindi wa mabao 4-0, yote yalitokana na kazi ya nyota hao watatu ambapo Chama alifunga mawili na kupiga pasi moja iliyozaa bao huku Luis akipiga pasi tatu za mwisho kwenye mechi hiyo.

Mchezo uliofuata ambao waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Gwambina FC, watatu hao walihusika na mabao mawili ambapo moja lilifungwa na Meddie Kagere baada ya kuunganisha kwa kichwa kona ya Luis na lingine lilifungwa na Pascal Wawa kwa ‘friikiki’ ambayo ilipatikana baada ya Bwalya kuchezewa rafu.

Katika mechi ambayo waliibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya JKT Tanzania, watatu hao walihusika moja kwa moja na mabao hayo manne ambapo Luis alifunga moja na kupiga pasi moja ya bao, Bwalya akitoaasisti mbili huku Chama akitoa asisti ya bao moja.

Lakini sio tu Morrison na Dilunga ambao wanapaswa kufanya kazi ya ziada ili kuweza kuwachomoa ama Chama, Bwalya au Luis katika kikosi cha kwanza bali pia nyota wengine ambao wana wakati mgumu ni Ibrahim Ajibu, Francis Kahata na Miraj Athuman ambao ndio huwa wanatumika kucheza katika nafasi za watatu hao.

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alisema ushindani wa namba uliopo ndio chachu ya wachezaji wake kufanya vyema kikosini.

“Kwangu mimi nafurahia kuona kila mchezaji anajitahidi kuitumia vyema nafasi ya kucheza anayopata kutoa mchango wenye faida kwa timu. Jambo la msingi ni wachezaji kuhakikisha wanatunza ubora na viwango vyao ili hiki wanachofanya kiendelee,” alisema Vandenbroeck.

Kwa upande wake Bwalya alisema pamoja na kuanza vizuri, anatambua ana jukumu kubwa mbele la kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri.

“Sina mengi ya kusema zaidi ni kufanya zaidi na zaidi ya nilichofanya. Huu ni mpira na unatakiwa utoe kila ulichonacho, uwe na muono, mazingatio na kufanya kazi kwa bidii ambapo siku zote vinalipa. Hivyo kikubwa ni kufanya kazi kwa bidii na kujitolea,,” alisema Bwalya.

Advertisement